Hata Yondani na Cannavaro? Duh!

Muktasari:

  • Bossou amekuwa katika kiwango cha juu Yanga ambapo katika mechi mbili alizokosa kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama na TP Mazembe, Yanga ilijikuta ikiruhusu mabao sita katika wavu wake.

KELVIN Yondani na Nadir Haroub Cannavaro ndiyo mabeki ambao Yanga wanawaaminia sana. Lakini Kocha wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa amesema mabeki wote nchini wanasubiri kwa Vicent Bossou na wajifunze mbinu kutoka kwake.

Mkwasa alisema Bossou anasaidia katika uongozi wa wachezaji ndani ya uwanja ambapo, hata makosa yakitokea ni rahisi kuyasahihisha kwani,  amekuwa akiwapanga wenzake vizuri na kupunguza hatari ya kuruhusu mabao, kitu ambacho bado ni changamoto kubwa kwa mabeki nchini.

Bossou amekuwa katika kiwango cha juu Yanga ambapo katika mechi mbili alizokosa kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama na TP Mazembe, Yanga ilijikuta ikiruhusu mabao sita katika wavu wake.

“Huwezi kusema moja kwa moja kuwa kukosekana kwa Bossou ndiyo sababu ya Yanga kuruhusu mabao mengi, lakini bado angeweza kuwepo na timu ikafungwa mabao mengi, kikubwa ni kuwa kuna kitu anaongeza kwenye timu. Ana uwezo mkubwa wa kuongoza wenzake uwanjani kama unavyofahamu soka ni mchezo wa makosa hivyo, kosa linapofanyika anakuwa makini kulisahihisha haraka,” alisema. Katika hatua nyingine Mkwasa alisema anafurahi kuona safu yote ya ushambuliaji ya Stars sasa itakuwa ikicheza soka la kulipwa ughaibuni jambo ambalo litawaongezea uwezo uwanjani. “Kwa kuanzia hawa washambuliaji tayari wananipa moyo, tutakuwa na wachezaji wengi zaidi ambao wamehusika katika mazingira magumu, wanaweza kuwa na msaada mkubwa kwetu. Ukweli uko wazi ukicheza nje unakuwa na vitu vya ziada, huwezi kuwa kama zamani,” alisema. Nyota wa Stars wanaocheza nje ni pamoja na Mbwana Samatta (KRC Genk), Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Elius Maguli (Dhofar FC) na Farid Musa anayekaribia kutua Hispania.