Chirwa atibua shavu la Kichuya

CHIRWA

Muktasari:

  • Chirwa,  raia wa Zambia tayari amefunga mabao matano mpaka sasa katika mechi nne mfululizo dhidi ya Mtibwa Sugar, Toto Africans, Kagera Sugar na JKT Ruvu na kuwafanya mashabiki waliokuwa wakimzomea kumshangilia.

STAA wa Simba, Shiza Kichuya anashikilia rekodi ya kufunga mabao katika mechi tano mfululizo za Ligi Kuu msimu huu, lakini rekodi hiyo tayari imeanza kunyemelewa na straika wa Yanga, Obrey Chirwa ambaye tayari amefunga katika mechi nne mfululizo mpaka sasa.

Kichuya aliweka rekodi hiyo kwa kuzifunga Azam, Majimaji, Yanga, Mbeya City na Kagera Sugar, lakini rekodi hiyo imekaribiwa kabisa na Chirwa, ambaye mwanzoni mwa msimu alikuwa akionekana kama garasa ndani ya Yanga.

Chirwa,  raia wa Zambia tayari amefunga mabao matano mpaka sasa katika mechi nne mfululizo dhidi ya Mtibwa Sugar, Toto Africans, Kagera Sugar na JKT Ruvu na kuwafanya mashabiki waliokuwa wakimzomea kumshangilia.

Awali, kabla ya kufunga bao lake la kwanza Ligi Kuu, Chirwa alikuwa amekaa nchini kwa miezi takribani mitatu bila kufunga bao jambo ambalo lilizua hofu huku mashabiki wakihoji  kama kweli ni straika ama ni beki.

“Ni mchezaji mzuri sana, mwanzo alikutana na changamoto ya ubora wa Donald Ngoma na Amissi Tambwe, lakini sasa naona ameanza kuingia kwenye mfumo,” alisema staa wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa.

“Nilipomtazama kwa mara ya kwanza nilifahamu ni mchezaji wa maana, tatizo alikuwa anataka kutengenezewa sana ndipo afunge, sasa naona anajiongeza, kupumzishwa kwa Ngoma pia kumekuwa faida kwake.

“Unajua mchezaji mzuri anaweza kushindwa kufanya vizuri katika mechi za mwanzo, lakini ukimvumilia atafanya vizuri tu, ni jambo la kheri kwa Yanga,” aliongeza Pawasa ambaye kitaaluma ni kocha.

Mzambia huyo kwa sasa anakamata nafasi ya tatu ya wafungaji akiwa sambamba na Omar Mponda wa Ndanda na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting waliofunga pia mabao matano.

Kichuya anaongoza orodha akiwa na mabao saba akifuatiwa na Amissi Tambwe wa Yanga na Rashid Mandawa wa Mtibwa Sugar wenye mabao sita kila mmoja.