Casillas aanza kupiga matizi mdogo mdogo

Thursday November 20 2014HUSSEIN Sharrif ‘Casillas’

HUSSEIN Sharrif ‘Casillas’ 

HUSSEIN Sharrif ‘Casillas’ kipa wa Simba aliyeumia ugoko kambini Afrika Kusini, ameanza mazoezi madogo madogo na baada ya wiki mbili ataanza kupiga mpira.

Casillas aliyesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Mtibwa Sugar, aliumia kambini Afrika Kusini ambako timu yake ilikuwa ikijiandaa kwa mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Oktoba 18.

Akizungumza na Mwanaspoti, Casillas alisema: “Nashukuru naendelea vizuri na tayari nimeanza mazoezi mepesi kujiweka vizuri ili nirudi uwanjani baada ya wiki mbili kuendelea na majukumu yangu.”

Kipa huyo alisema kwa wakati anafanya mazoezi mepesi ya kuimarisha sehemu iliyoathirika katika mguu wake na utakapoimarika ataanza mazoezi magumu kwa muda mfupi kisha atafanya mazoezi na Simba.

Baada ya kuumia, Casillas alifanya idadi ya makipa wa Simba walioumia kufikia wawili kwani awali Ivo Mapunda alikuwa majeruhi wa kidole. Hali hii ilisababisha Simba kumtumia Manyika Peter langoni dhidi ya Yanga na kutoka suluhu.

Hata hivyo, Casillas atakaporejea anatarajia kukutana na changamoto kubwa ya nafasi kwani Manyika anaonekana kukubalika na benchi la ufundi pia ujio wa Juma Kaseja kama mambo yakienda vizuri. Hata Ivo akibaki ni changamoto kwake.