Busungu huyoo Stand United

STRAIKA wa Yanga Malimi Busungu

Muktasari:

Kutokana na hilo Busungu amesema hana tatizo la kujiunga na Stand United ya Shinyanga ambayo imeonyesha nia ya kumsajili ikiwa tu watamalizana na Yanga.

STRAIKA wa Yanga Malimi Busungu hakufanikiwa kucheza mechi hata moja katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara uliomalizika mwezi uliopita.

Kutokana na hilo Busungu amesema hana tatizo la kujiunga na Stand United ya Shinyanga ambayo imeonyesha nia ya kumsajili ikiwa tu watamalizana na Yanga.

Busungu aliidokeza Mwanaspoti kuwa wiki iliyopita viongozi wa Stand walimfuata na kumweleza wanataka kumsajili lakini alichowajibu ni kwamba waende kuongea na uongozi wa Yanga kwani yeye bado ni mchezaji halali wa timu hiyo na bado ana mkataba.

“Ni kweli viongozi wa Stand walinifuata na wameniambia wanataka kunisajili lakini niliwajibu kuwa hilo suala lipo nje ya uwezo wangu kwani mimi bado ni mchezaji halali wa Yanga na kama kweli wananitaka basi waende kuongea na uongozi wa timu yangu,”alisema.

“Kama watakubaliana na uongozi wa timu yangu mimi nipo tayari na kiroho safi kwenda kukipiga katika timu hiyo kwani mpira ndio kazi yangu na ndiyo sehemu inayoendesha maisha yangu,” alifafanua.

Viongozi Stand ambao kwa sasa wanakabiliwa na ukata walisema wakishindwa kumsajili kwa dau atakalotaka watapambana kumpata kwa mkopo. Lakini kwenye mipango ya Yanga, jina la Busungu lipo kwa kocha George Lwandamina ambaye ameomba amuone kwanza.