Amewaumbua

Muktasari:

  • Kumbuka hii. Mabosi wa Simba waliapa kwamba msimu huu hawataki kabisa mchezaji wao yeyote wa kigeni asugue benchi, lakini tayari Mzamiru amefanikiwa kumuweka benchi Mussa Ndusha katika kikosi cha kwanza cha Kocha Joseph Omog, jambo ambalo linaonekana kuwa nishai kwa mabosi wake.

MSIMU huu Simba imefanya usajili kwa kushirikiana na nyota wake wa zamani ambapo, Ulimboka Mwakingwe alipewa nafasi ya kupendekeza nyota kadhaa na akaingia pale Mtibwa Sugar akawaibia kiungo mmoja anaitwa, Mdhamiru Yassin ambaye amefanya kitu ambacho kimeanza kuwaumbua mabosi wa Simba.

Kumbuka hii. Mabosi wa Simba waliapa kwamba msimu huu hawataki kabisa mchezaji wao yeyote wa kigeni asugue benchi, lakini tayari Mzamiru amefanikiwa kumuweka benchi Mussa Ndusha katika kikosi cha kwanza cha Kocha Joseph Omog, jambo ambalo linaonekana kuwa nishai kwa mabosi wake.

Katika mechi za ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu, Ndusha pamoja na Juuko Murshid walisugua benchi kuwapisha Mdhamiru pamoja na Method Mwanjali huku Blagnon Frederic akilazimika kumsubiri benchi Ibrahim Ajibu aliyeanza pia. Beki wa kulia, Javier Bokungu tayari ametemwa klabuni hapo.

Wakati huo huo katika kikosi cha Azam, Kocha Zeben Hernandez alianza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya African Lyon akiwa na wachezaji wawili tu wa kigeni ambao ni Jean Mugiraneza na Bruce Kangwa huku nyota wengine wakisugua benchi.

Nyota wa kigeni wa Azam ambao walikuwa fiti lakini wakalazimika kusugua benchi ni Kipre Bolou na Fransisco Zekumbariwa, ambaye amesajiliwa na timu hiyo akitokea City Boy ya Zimbabwe.

Nyota mpya Gonazo Bi Ya Thomas aliyejiunga na Azam akitokea Club African ya Ivory Coast bado hajawa fiti huku Sergie Wawa akiendelea na mazoezi mepesi baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu wakati beki mpya, Daniel Amoah bado hajajiunga na timu hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa Azam, Nassoro Idrissa ‘Father’ alisema Amoah atajiunga na wenzake kwa kuchelewa kutokana na timu yake ya zamani kuomba amalizie mechi za hatua ya Makundi ambapo, leo Jumanne timu yake ya Medeama itacheza ugenini na MO Bejaia ya Algeria.