Rooney, Pogba kumwachia kazi Zlatan Ibrahimovic

Muktasari:

“Nani anafunga sio jambo muhimu, cha msingi ni kushinda tu. ndiyo, nimefunga mabao matatu mpaka sasa katika Ligi Kuu England na nina furaha lakini huu ni mwanzo tu. msimu ni mrefu, nitafanya kazi kubwa, timu itafanya kazi kubwa na taratibu tutakuwa bora zaidi kwa hiyo tusubiri kuona matokeo yatakuaje.”

NI ngumu kuwaweka mafahari katika zizi moja. Ndicho kinachotokea Manchester United kwa sasa. Kununuliwa kwa mastaa wengi dirisha hili kumempa presha kubwa Kocha Jose Mourinho. Moja kati ya presha yake ni kuchagua mtu wa kupiga penalti za Man United.
Hata hivyo, Mourinho ametoa siri kwamba amewachagua wachezaji watatu wapige penalti. Nahodha Wayne Rooney, mchezaji ghali, Paul Pogba na mchezaji mwenye majivuno na kipaji kikubwa, Zlatan Ibrahimovic.
Pamoja na hao watatu, penalti inabidi ipigwe na mchezaji mmoja na Mourinho amepata nafuu baada ya kukiri kwamba Rooney na Pogba wamezungumza na Zlatan na kumpa jukumu la kupiga penalti za timu hiyo inayosaka kurudisha heshima.
Ijumaa usiku, Zlatan alipiga penalti ya Man United katika pambano dhidi ya Southampton na kufunga huku ikiwa ni bao lake la pili kwa mechi hiyo huku likiwa ni la tatu kwa msimu huu. Mourinho ameweka wazi siri ya penalti hiyo.
“Nimepanga watu watatu katika penalti, Paul, Wayne na Zlatan, lakini wakati mwingine napenda mchezaji anapojisikia ‘Hii penalti ni kwa ajili yangu’. Wayne na Paul wenyewe walimwambia Zlatan ‘Zlatan penalti inapokuja wewe ndio wa kwanza. Kama hautaki kupiga kwa sababu fulani basi sisi tupo, lakini wewe ndio mwenyewe. Walifanya maamuzi haya wenyewe,” alisema Mourinho.
Zlatan mwenyewe akiri kauli hiyo ya Mourinho kwa kudai kwamba alishaongea na Rooney kuhusu hilo wiki mbili zilizopita. “Tuliongea kama wiki mbili zilizopita kwa hiyo hakukuwa na tatizo. Tuliamua muda mrefu sana na haikuwa uwanjani.”
Wakati Mourinho akizungumzia kuhusu Penalti, Zlatan mwenyewe ameibuka na kuzipiga mkwara timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu ya England huku akidai kwamba United itwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England ifikapo Mei mwakani.
“Naamini tutatwaa ubingwa, nina mawazo hayo. Lakini tunahitaji kufanya kazi kubwa na tutafanya kila tuwezacho na kuzipiku timu nyingine ili tushinde. Kwa sasa nimejikita zaidi katika kuisaidia timu kushinda na baada ya mechi mbili tumeshinda mechi mbili,” alisema staa huyo wa kimataifa wa Sweden.
“Nani anafunga sio jambo muhimu, cha msingi ni kushinda tu. ndiyo, nimefunga mabao matatu mpaka sasa katika Ligi Kuu England na nina furaha lakini huu ni mwanzo tu. msimu ni mrefu, nitafanya kazi kubwa, timu itafanya kazi kubwa na taratibu tutakuwa bora zaidi kwa hiyo tusubiri kuona matokeo yatakuaje.”
Tayari mshambuliaji huyo mrefu mwenye umri wa miaka 34 ameanza kuwa gumzo katika viunga vya Old Trafford ambapo anabashiriwa kwamba huenda akaacha jina kubwa kama ilivyokuwa kwa akina Eric Cantona na Cristiano Ronaldo.
Zlatan amesema anataka kuwasaidia wachezaji wengine Old Trafford hasa wale chipukizi kuwa na roho za ushindi huku akijilinganisha mwenyewe alipotua Juventus mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 22 tu ambapo alikutana na wachezaji wababe waliomjengea ujasiri wa ushindi
“Nilicheza mastaa wakubwa, namaanisha nilipotua Juventus nikiwa mdogo. Kulikuwa na Vieira, Vieira, Cannavaro, Thuram, Buffon, Del Piero, Trezeguet, Nedved, Camoranesi, Emerson. Ilikuwa timu ya wababe. Kulikuwa na wachezaji wengi wakuwa na akili yangu ya ubabe niliipata hapo. Unakuwa umepevuka zaidi, nina watoto wawili na inabidi nichukue majukumu zaidi,” alisema Zlatan.