Muktasari:

Akizungumzia hilo Omog alisema, Muivory Coast huyo ambaye aliletwa nchini na kipa wa klabu hiyo ambaye pia ni raia wa huko, Vincent Agban, alipatwa na tatizo hilo ambalo linamfanya ashindwe kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake.


KOCHA Joseph Omog amewapiga panga Mcameroon mwenzake Serge Ndjack Anong na Mganda anayefahamika kwa jina la Keko, kitendo hicho kimemshtua straika kutoka Ivory Coast, Blagnon Frederick ambaye ameamua kuanza kujifua mwenyewe.

Ukiachana na tatizo la kiafya la kuugua mafua hivyo kuamua kujitenga, lakini straika huyo ni kama amejishtukia kimtindo kwamba anapaswa kuwa fiti kwelikweli ili kuweza kumshawishi Omog ambaye hajui kuremba kama mtu anamzingua.

Blagnon, amekuwa akifanya mazoezi hayo akiongozwa na meneja wa timu, Habas Ally na daktari, Yassin Gembe ambayo ni yale ya kukimbia pamoja na viungo.

Akizungumzia hilo Omog alisema, Muivory Coast huyo ambaye aliletwa nchini na kipa wa klabu hiyo ambaye pia ni raia wa huko, Vincent Agban, alipatwa na tatizo hilo ambalo linamfanya ashindwe kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake.

“Ameshindwa kufanya mazoezi na wenzake kwa sababu anasumbuliwa na mafua kidogo, atakapokuwa vizuri ataungana na wenzake,”alisema Omog.

Hata hivyo, Muivory Coast huyo, ambaye ni mrefu kwa umbo atakapopona, atakuwa na kibarua cha kumshawishi Omog amsajili baada ya kuweka msisitizo, anataka wachezaji imara na wenye uwezo kwa ajili ya Simba.


NIMUBONA 

ACHEMSHA 

Katika hatua nyingine beki wa zamani wa Simba, Mrundi, Emily Nimubona ameamua kurudi kwao Burundi baada ya kufanya tathmini na kujiridhisha kuwa Tanzania hakuna timu inayoweza kumsajili na kumlipa anachotaka baada ya mabosi wa Mbeya City waliomleta, kumzimia simu.

Nimubona aliyeichezea Simba msimu uliopita nafasi ya beki wa kulia, alitarajia kuondoka nchini Ijumaa iliyopita kwenda kwao Burundi baada ya kukwama jijini Dar es Salaam.

Alisema, kilichomfanya arudi Tanzania ni baada ya kuzungumza na mabosi wa City ambao walimhakikishia ajira, lakini baada ya kufika Dar es Salaam, ikawa kinyume.

Alipowataarifu uwepo wake ikawa tabu, kila alipopiga simu kuwatafuta, hawakupokea tena simu yake.