Simba, Yanga zapewa mchongo mechi za CAF

SIMBA na Yanga wikiendi hii zitakuwa kwenye majukumu ya kimataifa kwa kucheza mechi zao za kwanza za michuano ya CAF, lakini wadau wa klabu hizo wamezipa mchongo wa maana kama kweli zinataka kufika mbali kwenye mechi hizo.

Sekilojo Chambua aliyewahi kuichezea Yanga alisema anaziangalia mechi hizo kwa jicho pana na kuamini kuwa mastaa wa klabu hizo wakikomaa timu hizo zitapeta kiulaini, huku akiipa nafasi kubwa Simba ya Emmanuel Okwi na John Bocco.

Chambua alisema Simba, inaonekana kuwa na uhai kuliko Yanga, kuelekea katika mechi hizo za CAF, akisisitiza Okwi na Bocco kwa sasa wapo juu kisoka.

Yanga itaanza kazi Jumamosi kwa kuvaana na St Louis ya Shelisheli waliotua na kupiga tizi lao tangu jana asubuhi Uwanja wa Karume, kabla ya Jumapili kuwapisha Simba kucheza na Gendermarie Nationale ya Djibouti.

“Yanga ifanye kazi ya ziada, kwani licha ya kushinda dhidi ya Lipuli ya Iringa, haitoshi kujiona wana kazi rahisi, ndio maana ilitokea hata mashabiki kumzonga Katibu Mkuu wao Boniface Mkwasa, kuonyesha hawaridhika na aina ya uchezaji.”

“Ila naamini timu zote zikikomaa na hasa Simba kuwatumia Okwi na Bocco wanaweza kufanya kweli katika michuano ya mwaka huu, muhimu wachezaji wa timu zote kuwa na nidhamu uwanjani,” alisema Chambua.

Naye straika wa zamani wa timu hizo, anayeichezea JKT Mlale, Danny Mrwanda alisema Simba na Yanga, zinatakiwa zicheze kwa mtazamo wa kulibeba taifa, wakijua Watanzania wapo nyuma yao.

“Kwa Simba, kikosi chao kinaonekana kuwa imara, lakini wanahitaji kuongeza umakini na wawajenge roho ya uzalendo kwa timu na taifa, lakini Yanga wajengewe roho ya kujiamini na kuweka kando kama kuna vitu haviendi sawa,” alisema.

Kocha wa Dodoma Mji, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alizitazama Simba na Yanga, akisema wanapaswa kuwa na hamu ya kutaka kufanya kitu ndipo wanaweza wakawa na hatua nyingine.