Ni kweli namzimia kinoma Rich Mavoko

Thursday January 4 2018

 

By RHOBI CHACHA

MUUZA nyago wa video za muziki Bongo ambaye pia ni mwimbaji kwa sasa akitamba na nyimbo kadhaa kama ‘Usimwache’, ‘Utamu’, ‘Give It To Me’, Lulu Diva achana naye kabisa.

Mwanadada huyo ambaye majina yake kamili ni Lulu Abbas ni mmoja ya wasanii wanaosumbua nchini kwa mwonekano wake na hata kazi yake ya sanaa.

Mwanaspoti lilimnasa na kupiga naye stori mbili tatu na kufunguka mambo kadhaa ambayo huenda baadhi ya mashabiki wake hawakuwa wanayafahamu.

Tiririka naye.

MWANASPOTI: Kitu gani ulichowahi kukifanya na unajutia mpaka sasa?

LULU DIVA: Kumjibu mtu aliyenitukana, yaani najutia hadi leo kwani nimejiona ni mjinga kumjibu mtu ambaye hakustahili kujibiwa.

MWANASPOTI: Ulishawahi kulala nje ya nyumba unayoishi?

LULU DIVA: Ndio, mara kadhaa nimelala nje hasa ninapokuwa na shoo mikoani, ila nikiwa hapa hapa Dar sijawahi kabisa.

MWANASPOTI: Kitu gani wewe hukipendi?

LULU DIVA: Sipendi kuwa na marafiki ama kukusanyika katika mikusanyiko ya watu.

MWANASPOTI: Inasemekana umaarufu umekufanya uanze kutumia mkorogo ni kweli?

LULU DIVA: Yaani hili swali naulizwa kila sehemu. Sijawahi kutumia mkorogo labda huu weupe watu wanaouona ni kwa ajili ya mekapu na setingi ya simu ukitaka kupiga picha. Ila kwa kweli situmii hiyo kitu kabisa.

MWANASPOTI: Umeolewa?

LULU DIVA: Hapana, ila ninaye mpenzi.

MWANASPOTI: Ukikutana na mpenzi wako unapenda kumwambia nini?

LULU DIVA: Nitamwambia ili tuweze kuishi miaka mingi kimapenzi, asichepuke na asiwe muongo, maana wanaume wa kibongo wengi wao waongo wadanganyifu.

MWANASPOTI: Una mpango wa kujiingiza katika siasa?

LULU DIVA: Weee!!! Hapana kabisa, sipendi siasa hata kidogo.

MWANASPOTI: Ukiwa unaendesha gari, kitu gani hupendi kukutana nacho barabarani.

LULU DIVA: Ile alama ya stop na matuta. Kwa kweli matuta nayachukia sana.

MWANASPOTI: Kwa nini unapenda kuvaa nguo fupi na za kubana?

LULU DIVA: Huwa zinanifanya nijione huru na pia zinanipendeza sana.

MWANASPOTI: Kitu gani unapenda kufanya kwenye simu yako?

LULU SPOTI:Napenda sana kuchati, ndio maana simu yangu kila muda inakuwa na chaji. Ikiwa haina chaji huwa naumia sana.

MWANASPOTI: Una mpango wa kuacha muziki?

LULU DIVA: Jamani ndio kwanza nimeanza, mara tu niache, hapana sina mpango kwa sasa, sijui mbele ya safari itakuwaje.

MWANASPOTI: Kwa nini hupendi kuweka wazi mahusiano yako ya mapenzi?

LULU DIVA: Sipendi tu mambo yangu binafsi kuyaweka hadharani.

MWANASPOTI: Huoni ni kero kupakaziwa unatoka mara na huyu, mara yule kwa vile hupendi kumwanika mpenzi wako hadharani?

LULU DIVA: Mie naona safi tu, ndio napenda maana hawana uhakika na wanachosema na yote hiyo sababu huwa sipendi kuanika mambo yangu hadharani.

MWANASPOTI: Inasemekana unampenda Rich Mavoko kuliko wanaume wote wa kibongo?

LULU DIVA: Hahahaha nilijua tu utaniuliza swali kuhusu Mavoko. Niseme ukweli Rich Mavoko nampenda kama wanaume wengine ninavyowapenda. Isitoshe Mavoko ni rafiki yangu wa karibu sana, sema watu wanahisi pengine ndiye ninayetoka naye.

MWANASPOTI: Tutarajie nini kimuziki 2018?

LULU DIVA: Naomba tu mashabiki wangu wakae mkao wa kula, nawashukia na kazi mpya ambazo watazifurahia na kuridhika nazo. Kifupi sitawaangusha.