Mtibwa yazitibulia Yanga, Singida

Muktasari:

  • Mtibwa ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa na kufikisha pointi 24 na kukwea hadi nafasi ya tatu ikiishusha Singida yenye alama 23 na Yanga iliyoporomoka hadi nafasi ya tano ikiwa na pointi zao 21 baada ya kucheza mechi 12.

MTIBWA Sugar kweli ubingwa inautaka msimu huu baada ya jana Jumamosi kushinda ugenini bao 1-0 dhidi ya Lipuli na kuzitibulia Yanga na Singida United zilizoporoka kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Mtibwa ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa na kufikisha pointi 24 na kukwea hadi nafasi ya tatu ikiishusha Singida yenye alama 23 na Yanga iliyoporomoka hadi nafasi ya tano ikiwa na pointi zao 21 baada ya kucheza mechi 12.

Bao la kipindi cha kwanza la Hassan Dilunga lilitosha kuisaidia Wakata Miwa hao kuzidi kuzipa presha timu zilizopo juu ikionyesha nia yao ya kuutaka ubingwa iliyowahi kuutwa mara mbili mfululizo mwaka 1999 na 2000.

Lipuli ambayo inaendelea kuishi maisha magumu bila nahodha wake, Asante Kwasi kaliyehamia Simba, kwa kipigo hicho imesalia na alama zao 14 ikishuka hadi nafasi ya nane kutoka ya saba iliyoiachia Mbao iliyotoka sare ya 1-1 na Ndanda FC.

Katika mchezo huo, Nassoro Kapama aliiokoa Ndanda na kipigo baada ya bao la kusawazisha la dakika ya 65 ikifuta uongozi wa wageni waliopata bao la mapema dakika ya 37 kupitia straika Mrundi, Emmanuel Mveyekule kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Nao Chama la Wana, Stand United ikiwa nyumbani ilijinasua mkiani kwa kuilaza Ruvu Shooting bao 1-0, shukrani kwa straika mpya Bigirimana Babikakule aliyefunga katika dakika 47.

Stand United sasa inashika nafasi ya 15, ikiiachia msala Njombe Mji ikiburuza mkia na alama zao nane itakayoikaribisha Kagera Sugar kesho Jumapili mjini Njombe.