Chirwa amtumia salamu Okwi

Muktasari:

Yanga ndiyo timu iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nyingi zaidi tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo

Dar es Salaam. Mkubwa ni mkubwa tu. Hakuna ubishi sasa, Yanga imezidi kuthibitisha kwamba ndio timu kubwa zaidi nchini. Inafanya kile ambacho watu hawajakitazamia.
Ikiwa na majeruhi zaidi ya 10, Yanga imeshinda mechi za tatu za ligi mfululizo jana wameichapa Njombe Mji mabao 4-0, pia ilivunja mwiko mjini Iringa na kuifunga Lipuli mabao 2-0 na awali wakaiduwaza Azam nyumbani kwake kwa kuifunga mabao 2-1.
 Inafurahisha sana.
Imefikia hatua Yanga imeishiwa mabeki wa kati na kwenye mechi ya iliyopita, ilimchezesha Said Juma 'Makapu' kwenye nafasi hiyo lakini haikuruhusu bao. Huwa inatokea mara chache sana.
Mabeki wa kati, Nadir Haroub 'Cannavaro', Andrew Vincent 'Dante' na Abdallah Shaibu wote ni wagonjwa. Yule beki wao Mkongomani, Fiston Kayembe bado hajapata hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC). Nani angecheza nafasi hiyo? Ilibidi awe Makapu.
Upande wa pili, kwenye benchi Yanga ilikuwa na kipa chipukizi, Ramadhani Kabwili ambaye alilazimika kuanza dhidi ya Njombe mji ikiwa ni siku tatu tangu alipoingia dakika ya 15 baada ya kipa namba moja, Youthe Rostand kuumia. Nani aliwahi kuwaza kwamba Kabwili anaweza kudaka mechi ya Ligi Kuu bila kuruhusu bao? Imetokea pale Iringa na Dar es Salaam.
Kipa namba mbili, Beno Kakolanya naye ni mgonjwa. Yanga inalazimika kutumia wachezaji waliopo. Wachezaji hawashindanii nafasi tena kwani wengi ni majeruhi.
Ushindi huo wa Yanga unatoa taswira mbili. Kwanza, wadau wa soka nchini wasiibeze kwani inaweza kupunguza wigo wa pointi baina yake na Simba muda wowote. Pili, wachezaji wa Yanga wanajitambua na wanafahamu wapo kwenye hali gani. Wanacheza kwa ajili ya timu.
Pamoja na yote, Pius Buswita na Obrey Chirwa wamezidi kuwa watamu. Kazi waliyoifanya kwenye mchezo huo, inazidi kuwapandisha chati. Buswita amezidi kuwa mbunifu. Wakati Chirwa amefikisha mabao 10 na kumtishia Emmanuel Okwi wa Simba mwenye mabao 12.

BOCCO SI WA MCHEZO
Watu wa soka wana maneno sana. Huko mtaani wanasema kuna vitu viwili tu vinavyojua kufunga zaidi nchini. Ni waumini wa dini na John Bocco. Jumapili alikuwa akifunga bao lake la tisa Ligi Kuu kwa msimu huu.
Alifunga bao maridadi la kwanza kwa kichwa huku akiwa amekumbatiwa na mchezaji wa Ruvu Shooting. Akafunga bao la pili kwa akili kubwa, akiiadhibu safu ya ulinzi ya Ruvu iliyokuwa imeparanganyika. Huyu ndiye Bocco tunayemfahamu. Anafunga popote anapoamua kufanya hivyo.
Bocco wa sasa amekuwa moto. Amefunga mabao matano katika mechi nne za mwisho alizocheza. Inapendeza sana.
Upande wa pili, safu ya ulinzi ya Simba imezidi kuwa tamu. Imecheza mechi tano mfululizo za Ligi Kuu bila kuruhusu bao. Aishi Manula amefikisha mechi 11 bila kuruhusu bao msimu huu. Rekodi tamu.


KAGERA MAMBO YAMEGOMA
Hakuna namna tena. Ni bora Kocha Mecky Maxime akaachia ngazi Kagera Sugar ili kulinda heshima yake. Hali ya timu hiyo kwa sasa ni mbaya. Jumapili ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mbao FC. Inasikitisha sana.
Mambo ni kama yamemgomea kabisa Maxime. Kila analofanya sasa linagoma. Amejaribu kurekebisha kila kitu, lakini mambo yamegoma. Nini kimempata Maxime?
Kabla ya mechi hiyo walikaa kikao ili kujadili kilichowasibu. Hata hivyo kikao hicho hakijawasaidia. Kagera inahitaji kufanya maamuzi magumu kwani timu hiyo inaweza kushuka daraja, kama utani vile. Kwa sasa ipo nafasi ya 13 na pointi 13 sawa na Njombe Mji iliyopo mkiani.


SINGIDA IMEIMARIKA
Wakati mwingine mambo huwa yanatokea haraka sana. Kwenye mchezo wa Singida United na Mwadui, baada ya dakika 32 tu, Singida ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 pale Namfua. Ilikuwa jambo la kushtua.
Mwadui ilikuwa moto. Ilikuwa imeishika Singida kila idara. Mechi ilionekana kama imekwisha mapema kabisa.
La haula! Matokeo ya mwisho, Singida ilikuwa imeshinda kwa mabao 3-2. Inafurahisha sana. Singida haikukubali kufungwa kirahisi. Ilitulia na kuanza kushambulia. Iliongeza pia nidhamu kwenye kukaba.
Ilipata bao la ushindi kwenye dakika za nyongeza. Ni wazi kwamba morali yao ilikuwa juu. Ni mechi ya pili sasa wanashinda kwa bao la usiku. Wiki moja nyuma iliifunga Prisons kwa bao la dakika za nyongeza pia.


USHAMBULIAJI AZAM FRESH
Azam ilianza msimu huu ikiwa na safu mbovu ya ushambuliaji. Ilicheza kwa miezi mitatu bila kufunga mabao mawili kwenye mchezo mmoja. Mara nyingi ilishinda kwa bao 1-0. Ilistaajabisha sana.
Kwa sasa mambo yanaonekana kuwa tofauti kidogo. Azam imeimarika kwenye safu hiyo ya ushambuliaji. Imefunga mabao sita kwenye mechi zake tatu za mwisho. Ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda unaonyesha kwamba safu yao ya ushambuliaji sasa imekuwa tamu.
Ikiendelea na kasi hiyo inaweza kurudisha ule ushindani wake wa karibu na Simba. Ianze kwa kuifunga Simba leo Jumatano.