Mkomola apewa masaa 38 Yanga

Muktasari:

Mkomola ameumia katika mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting waliyoshinda bao 1-0 ,  Uwanja wa Taifa, mchezo ambao ulikuwa wake wa kwanza ligi kuu anaanza.

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Yohana Mkomola amepewa muda wa masaa 38 ya mapumziko  akae bila kugusa mpira  lakini mwenyewe,  amewatoa wasiwasi mashabiki wake na wa klabu hiyo kuwa anaendelea vizuri.

Mkomola ameumia katika mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting waliyoshinda bao 1-0 ,  Uwanja wa Taifa, mchezo ambao ulikuwa wake wa kwanza ligi kuu anaanza.

Daktari wa Yanga, Edward Bavu amesema, Mkomola ameumia enka na sasa anaendelea vizuri:

"Kama mlivyoona siku ile ya mchezo alishindwa kumaliza kwa sababu ya maumivu ya enka, tumempa

muda wa mapumziko wa masaa 38 akae tu ajiangalizie na baada ya hapo, tutajua tuendelee na programu ipi ya matibabu."

"Unapokuwa na mchezaji mwenye maumivu, kitaalamu kupona inategemea na umri na hivyo,

Mkomola bado damu changa, tunaamini atarudi kwa wakati,"anasema Bavu na kufafanua juu ya

mchezo wao ujao wa Azam amsema.

"Ni ngumu kuuzungumzia kwa sasa kuwa atacheza au hatacheza kwa sababu bado kuna muda, pia

kucheza kwake inategemea, Yanga ina wachezaji wengi kama yeye ameumia wapo wengine

watacheza."

Kwa upande wa Mkomola ambaye baada ya kuumia, alikuwa na masikitiko ikiwa ni mchezo wake wa

kwanza wa ligi kuanza dakika za mwanzo na anapata matatizo hayo amesema: "Kwa sasa naendelea vizuri, nimeambiwa nikazane na barafu na dawa, nitakuwa sawa."

"Yote ni mipango ya Mungu, ndiyo nimeanza kupata nafasi ya kuanza ningekaza, huenda mambo yangu yangekuwa mazuri zaidi lakini ndiyo hivyo tena,"anasema.