Mburundi aliyesaini Njombe kimaajabu

Muktasari:

  • Maisha ya klabu hii sio ya kuridhisha sana kutokana na ukata huku suala la mishahara na pesa za usajili kwa wachezaji ikiwa ni ishu kubwa.

USISHTUKE! Ni hali halisi hiyo, klabu ya Njombe Mji licha ya kwamba ndio kwanza imepanda daraja msimu huu, lakini ina wachezaji kutoka Cameroon, Burundi na Nigeria.

Maisha ya klabu hii sio ya kuridhisha sana kutokana na ukata huku suala la mishahara na pesa za usajili kwa wachezaji ikiwa ni ishu kubwa.

Mwanaspoti lilizungumza na mchezaji Lewis Harerimana, raia wa Burundi ambaye katika dirisha dogo alitua nchini na kujiunga na Njombe Mji akitokea klabu ya Mukura ya Rwanda.

KWANINI NJOMBE

Harerimana alisema alikuwa haifahamu kabisa Njombe Mji, lakini wakala wake ndio alimwambia anahitajika kuja Tanzania kuna timu ambazo zinahitaji huduma yake.

“Sijawahi kuisikia Njombe hata siku moja, wakala alineleza kuna timu imepanda ligi kuu Tanzania hivyo, nahitajikakuja kucheza nikasema ngoja niende kufanya kazi, hapa nazifahamu Simba, Yanga na Azam,” alisema.

Hata hivyo, alisema alivyofika badala yake wakala huyo akawa anamtafutia timu nyingine huku ikionekana kama alimleta, huku akiwa hafahamu ni klabu gani huyo atasaini.

BARIDI YEYE FRESH TU

Wachezaji wengi wa kigeni wakienda nchi nyingine wanasumbuliwa na hali ya hewa kutokana na mazingira kuwa tofauti, lakini kwa mchezaji huyu hali ni tofauti kwani ameonyesha kukomaa na baridi la Njombe.

“Baridi lipo nimeshalizoea kwa sababu hata Burundi muda mwingine huwa na baridi vile vile, huku muda mwingi baridi na kama hakuna baridi basi kutakuwa na upepo mkali,” alisema.

“Kwenye baridi ukiwa unacheza mechi au unafanya mazoezi huchoki haraka kwa sababu hewa huwa nyepesi, kwenye joto hewa inakuwa nzito unaweza ukachoka tu ghafla,”

NJOMBE KAFIKA?

Harerimana anasema katika klabu ya Njombe sio kwamba amefika, badala yake anatumia sehemu hiyo kama njia ya kujitangaza na kusonga mbele.

“Kwa mchezaji wa kulipwa huwezi ukasema upo sehemu moja kwa muda mrefu, labda kama itakupa kila kitu, nazungumzia makombe na vitu vingine, lakini kama sio hivyo lazima uondoke kuvitafuta na ndio kwangu ipo hivyo,”.

Aliongeza kwamba mipango yake ni kucheza moja ya klabu kubwa nchini, ili aweze kuonekana kisha kupata ulaji katika nchi nyingine ambazo vilabu vyake vinashiriki mashindano makubwa.

“Hapa bado sijafika kabisa kwenye malengo yangu, natakiwa nicheze klabu inayoshiriki michuano mikubwa kutoka nje, nikicheza katika moja ya timu kubwa hapa sitokaa muda mrefu naondoka,” alisema.

LIGI YA BONGO NGUMU

Wachezaji wengi wa kibongo wamekuwa wakiona Ligi yao nyepesi, lakini Harerima anasema ni ngumu na inabidi utumie nguvu nyingi kucheza kutokana na kukamiana.

“Hapa ligi ni ngumu kuliko Rwanda, kule ufundi mwingi kuliko nguvu, halafu hapa wachezaji wanakuwa na wewe muda wote wakitumia nguvu,” anasema.

AKIPIGA NA MASOUD DJUMA

Kama ulikuwa hujui basi ni hivi, mchezaji huyu alikuwa katika kikosi kimoja na kocha msaidizi wa Simba Masoud Djuma, huku kocha wao akiwa Ally Bizimungu, kocha wa Mwadui fc.

“Nilicheza na Masoud tukiwa pale Inter Stars, mwalimu alikuwa ni Bizimungu, nafurahi tumekuja kukutana katika ligi moja huku kila mtu akiwa katika majukumu yake,” alisema.

KUMBE MUUZA MAGARI

Chirwa aliwahi kuweka picha katika mtandao ukimuonyesha analima, wengi walimbeza na kuona amefulia, lakini wachezaji wengi wamekuwa wakijihusisha na biashara nje ya soka ili maisha yao yasonge.

Harerima anajihusisha na biashara ya kuuza magari, akipata pesa yake ya usajili huwa anaigawanya na kufanya biashara hiyo akisaidiana na mkewe.

“Katika timu zangu zote ambazo nimepita hela ya usajili huwa naagiza gari Dubai kisha nauza Burundi, ni biashara ambayo inalipa na ilikuwa inamsaidia mke wangu kuendesha maisha yake nyumbani,” alisema.

AZIBWA MASIKIO NA MKEWE

Madem wa kibongo kama walikuwa wanaanza kummendea kiraka huyu wa Njombe Mji, basi imekula kwao kwa kuwa hana mpango nao zaidi ya kumheshimu mkewe.

“Kaka nimeoa, nina mke ambaye namheshimu sana, japo yeye yupo Burundi lakini haiwezi kunifanya nikamsaliti, nampenda mke wangu,”

AMKATAA TAMBWE, AMKUBALI MAVUGO

Straika Amis Tambwe anayekipiga Yanga, hivi sasa anasumbuliwa na majeraha ya goti, lakini Harerimana aliweka wazi kwamba mchezaji huyo umri umekwenda baada ya kucheza kwa muda mrefu.

“Nilicheza na Tambwe Eagle Noire nadhani ilikuwa 2006/7, lakini sasa hivi amekuwa mkubwa, kipindi kile nilikuwa mdogo sana, Mavugo ni straika mzuri hata akiwa timu ya Taifa anafanya vizuri.

Mavugo soka la hapa limemkataa na hii huwa inatokea kwa kila mchezaji, lakini kiukweli ni mchezaji mzuri na hilo ndio lililofanya mpaka atue hapa bila shaka baada ya kufanya vizuri.