Duh! Kumbe Ismail Juma aliacha mamilioni ya Ulaya

Tuesday February 13 2018

 

By Yohana Challe

Arusha. Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limekabidhi kiasi cha Sh6.8 milioni kwa familia ya mwanariadha Ismail Juma aliyefariki mwishoni mwa mwaka jana kwa ajali ya gari ikiwa ni fedha alizoziacha nje ya nchi wakati akishiriki mbio mbalimbali enzi za uhai wake.


Katibu Mkuu wa RT Wilhelm Gidabuday alisema fedha hizo walizipata kutoka kwa aliyekuwa meneja wake anayeitwa Gianni Demadonna raia wa Italia ambaye alikua amesaini mkataba na marehemu Ismail kwa ajili ya kumtafutia mashindano nje ya nchi.


"Jukumu la RT ni kuhakikisha inatetea haki na masilahi ya wanariadha hayapotei bila kujali yupo hai au amefariki hilo ndilo jukumu letu kama shirikisho," alisema Gidabuday.


Aliongeza kuwa baada ya kifo cha Ismail RT iligundua kuna fedha zake nje ya nchi na ndio walipoagiza fedha hizo zitumwe haraka kupitia shirikisho ili wazazi wake waone faida ya kazi aliyokuwa akifanya mtoto wao.


"RT ilimtuma mjumbe kwa mama mzazi wa Marehemu na kumweleza juu ya jasho la mtoto wake ambalo kwa fedha za kigeni ilikuwa Euro 2,584 sawa na Sh6,801,200 mil na tayari amepewa mama hiyo."

Gidabuday aliwaonya wanariadha kuacha kuwa na siri juu ya ukweli wa maisha yao halisi baada ya kugundua aliyekua anaishi na Ismail hakua mzazi wake na ndiye aliyekuwa akichukua fedha zote huku wazazi wake wakitaabika.


Aliongeza kuwa hata siku aliyofariki Ismail zilitumwa fedha kiasi cha $4,000 sawa na sh 8,800,000 Mil na hadi leo hakuna anayejua fedha hizo zilipotelea wapi.