Kwasi sasa aitaka namba ya Kichuya

Muktasari:

Kichuya amefunga mabao 18 kwenye kipindi hicho na kufuatiwa na Emmanuel Okwi mwenye 10, yote akiwa amefunga msimu huu tu.

BEKI wa kati wa Simba, Asante Kwasi, amesema huwa anafurahi zaidi kucheza winga, nafasi ambayo kwa sasa imeshikwa na Shiza Kichuya ambaye ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo kwenye kipindi cha miezi 18 sasa.

Kichuya amefunga mabao 18 kwenye kipindi hicho na kufuatiwa na Emmanuel Okwi mwenye 10, yote akiwa amefunga msimu huu tu.

Kwasi alisema nafasi hiyo inamfanya aweze kufunga zaidi ambapo sasa amefikisha mabao matano Ligi Kuu, moja pungufu ya Kichuya. Kwasi alifunga manne akiwa Lipuli na moja Simba.

Hata hivyo, Kwasi amekuwa akitajwa kufunga mabao sita, akijumuishiwa na lile la kujifunga la mchezaji wa Mbao FC, Robert Ndaki.

Kwasi aliyesajiliwa Simba akitokea Lipuli FC ya Iringa amefikisha idadi ya mabao hayo baada ya juzi Alhamisi kutupia kambani bao moja wakati Simba ikiishindilia Singida United mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kwasi alisema kuwa moja ya malengo yake kwenye ligi ni kuwa miongoni mwa nyota wanaofunga mabao mengi, lakini kubwa ambalo linaweza kumfanya afunge zaidi ni kucheza nafasi ya winga ambayo kwake ni rahisi kupanda na kufunga ingawa kucheza beki nako anamudu vyema.

“Nataka kuwa mfungaji bora, naamini naweza kufanya hivyo kwani huwa nafurahi zaidi nikicheza wingi na ndiyo maana hata nikipangwa kwenye nafasi yangu ya beki huwa nafunga kwani nina uwezo wa kupanda na kufanya mashambulizi nikitokea kwenye nafasi ya winga,” alisema.

“Siwezi kusema idadi ya mabao ambayo naweza kufunga msimu huu, ila kwa ufupi nitafunga mabao mengi tu ambayo yatasaidia pia kuifikisha Simba sehemu nzuri.”

Akimzungumzia mchezaji huyo, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema: “Nilipomwona Kwasi siku ya kwanza niligundua kuwa yeye si beki bali ni winga, nilimwita na kumuuliza huwa anapenda kucheza nafasi ipi akasema winga.

“Hivyo naamini kote huko alikopita Kwasi walikuwa wamembadili kucheza beki wakati yeye ni winga.”