Kwa mpango huu! Liverpool inunue tu Southampton

Muktasari:

Juzi Jumapili, Liverpool ilikutana na Southampton huko St Mary’s na kushinda 2-0, lakini hilo limeelezwa limefanikiwa kwa sababu Kop kwa Saints ni kama shambani kwao tu, wanakwenda kujichumia matunda kwa kadiri wanavyotaka.

LIVERPOOL, ENGLAND. UMESIKIA hii? Liverpool wameambiwa hivi ni bora tu wakaamua kuinunua klabu ya Southampton kuliko pesa wanazotumika kunasa wachezaji wa timu hiyo baada ya kutumia Pauni 175 milioni kupata huduma ya mastaa sita kutoka kwenye timu katika miaka ya karibuni.

Juzi Jumapili, Liverpool ilikutana na Southampton huko St Mary’s na kushinda 2-0, lakini hilo limeelezwa limefanikiwa kwa sababu Kop kwa Saints ni kama shambani kwao tu, wanakwenda kujichumia matunda kwa kadiri wanavyotaka.

Kwenye mechi hiyo kulitarajiwa kuona kikosi cha Liverpool kikiwa na mastaa kibao iliyowasajili kutoka Southampton.

Unajua kwanini Liverpool wameambiwa ni bora tu wangeinunua jumla Southampton kuliko kutumia pesa nyingi kusajili wachezaji wa timu hiyo ni baada ya klabu hiyo kuuzwa kwa Mchina, Gao Jisheng, ambaye alinunua asilimia 80 za hisa za timu hiyo kwa Pauni 210 milioni tu.

Kwa pesa ilizotumia Liverpool kusajili mastaa wa timu hiyo, Pauni 175 milioni kuifikia Pauni 210 milioni bado pesa kidogo tu, Pauni 35 milioni tu. Ndiyo maana wakaambiwa bora wainunue Southampton tu kuliko kupigwa pesa ndefu za kusajili wachezaji. Kwa misimu ya karibuni, Liverpool imewabeba mastaa kibao kwa pesa nyingi kutoka Southampton ikiwamo Dejan Lovren, Adam Lallana, Sadio Mane na Virgil van Dijk.

Wachezaji wengine ni Rickie Lambert na Nathaniel Clyne, ambao wameifanya Liverpool iwe imetumia mkwanja unaovuka Pauni 170 milioni. Unaambiwa thamani ya jumla ya klabu hiyo inaweza kufikia Pauni 260 milioni. Hebu cheki Liverpool ilivyopigwa pesa zao na Southampton kutokana na mastaa iliyowasajili kutoka kwenye timu hiyo.

Rickie Lambart, Pauni 4milioni

Straika Rickie Lambert alikuwa mchezaji wa mwanzo mwanzo kabisa kutoka Southampton kwenda Liverpool wakati aliponaswa kwa ada ya Pauni 4 milioni. Uhamisho huo ulikuwa ni ndoto zilizotimia kwa Lambert, ambaye alikuwa akiwaza siku moja kwenda kuichezea timu hiyo yenye maskani yake huko Anfield. Hata hivyo, mambo ya uwanjani hayakuwa mazuri kwa Mwingereza huyo baada ya kufunga mabao mawili tu katika mechi 25 alizocheza kwenye Ligi Kuu England.

Adam Lallana, Pauni 25milioni

Adam Lallana ni bonge la staa na ni mmoja wao waliotoka Saints na kwenda Liverpool katika kipindi cha karibuni. Kiwango chake bora huko St Mary’s kiliwafanya Liverpool kuzama mifukoni na kutoa Pauni 25 milioni kupata huduma ya kiungo huyo wa Kingereza. Licha ya kwenda kucheza kwenye kikosi kilichojaa mastaa wa maana kama Luis Suarez, Philippe Coutinho na Mohamed Salah, Lallana hajawahi kukwazwa na hilo na kiwango chake kinaonekana wazi.

Dejan Lovren, Pauni 20milioni

Beki wa kati, Dejan Lovren amekuwa na maisha yenye mchanganyiko wa mambo mengi huko Liverpool tangu alipotua akitokea Southampton. Amekuwa akifanywa kafara kutokana na matokeo mabaya inayopata timu hiyo ambayo moja kwa moja yamekuwa yakihusishwa na safu ya mabeki, na hasa kwenye eneo lake la beki ya kati.

Hakika alipokuwa Southampton alikuwa matata kweli, alikuwa beki kisiki na pengi hilo ndilo lililowafanya Liverpool kutoa Pauni 20 milioni kumsajili.

Nathaniel Clyne, Pauni 12.5milioni

Anapokuwa fiti, hakuna beki mwenye uwezo wa kutunza kiwango chake na kuwa bora kwa muda mrefu katika kikosi cha Liverpool kuliko Nathaniel Clyne.

Huyu ni mchezaji mwingine kutoka Southampton, ambaye huko kwenye kikosi cha Liverpool mchango wake umekuwa adimu kwa siku za karibuni kutokana na kusumbuliwa na majeraha. Hata hivyo, Clyne bado anahesabika kama mmoja wa mabeki bora kabisa kwenye kikosi cha Liverpool.

Sadio Mane, Pauni 34milioni

Sadio Mane anaelezwa ni mmoja kati ya wachezaji waliobora kabisa kwenye kikosi cha Liverpool ambao, iliwanasa kutoka Southampton. Kama isingekuwa ujio wa Mohamed Salah kwenye kikosi hicho cha Anfield, basi Mane angekuwa tegemeo kubwa la Liverpool kwenye mechi zao mbalimbali za Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ubora wake wa uwanjani kwa kushirikiana na washambuliaji wenzake, Salah na Roberto Firmino umeifanya Liverpool kuwa tishio.

Virgil van Dijk, Pauni 75milioni

Kwa sasa, Mdachi Virgil van Dijk ndiye mchezaji ghali zaidi kwenye kikosi cha Liverpool kwa sasa baada ya usajili wake wa Januari kuigharimu timu hiyo Pauni 75 milioni ilipomsajili kutoka Southampton. Juzi ilikuwa mechi yake ya kwanza kwa Van Dijk kucheza dhidi ya timu yake ya zamani akiwa kwenye jezi za Liverpool.

Si usajili mbaya sana baada ya kufunga mabao na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora katika mechi yake ya kwanza kuichezea Liverpool.