Kwa hili Yanga imeonyesha ukomavu

Muktasari:

  • Katika mzozo huo ilifikia mahali wanachama wa klabu hiyo kutishia kufanya maandamano ili kulazimisha serikali kuwapa nafasi kwa madai wanajisikia aibu kuchekwa kwa kukosa hata uwanja wa mazoezi wakati klabu yao imezaliwa miaka mingi iliyopita.

KWA muda mrefu klabu ya Yanga ilikuwa kwenye malumbano na Manispaa ya Ilala, ikishinikiza kuruhusiwa kupewa kibali cha kujenga Uwanja wa kisasa kwenye eneo la makao yao makuu iliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Katika mzozo huo ilifikia mahali wanachama wa klabu hiyo kutishia kufanya maandamano ili kulazimisha serikali kuwapa nafasi kwa madai wanajisikia aibu kuchekwa kwa kukosa hata uwanja wa mazoezi wakati klabu yao imezaliwa miaka mingi iliyopita.

Hata hivyo, pamoja na vitisho vyote, Manispaa ya Ilala iliendelea kushikilia msimamo wake ikiitaka Yanga isahau habari ya kujenga uwanja na majengo mengine kwenye eneo hilo kutokana na ukweli eneo la Jangwani ni hatarishi kimazingira.

Yanga ilikuwa ikishinikizwa kutafuta maeneo ya nje ya mji kama walivyofanya watani zao, Simba waliokwenda kununua kiwanja Bunju ama Azam waliokimbilia mapema eneo la Mbande, Chamazi wilayani Temeke.

Hata hivyo, baada ya kutafakari kwa kina na kuangalia ukweli ulivyo, Yanga iliamua kutuliza akili na kufanya jambo ambalo kwa makini ni kuonyesha ukomavu na usikivu baada ya kuamua kusaka eneo huko Kigamboni.

Yanga imepewa ardhi na Mwenyekiti wao, Yusuf Manji aliyemega sehemu ya eneo la hekta 712 analomiliki, ili klabu hiyo ijenge uwanja wake na kumaliza kelele zisizoisha za kushinikiza kujenga uwanja eneo la Jangwani ambako ilikuwa vigumu kufanikiwa.

Jana Jumatano klabu hiyo ilizindua eneo hilo kwa kuweka jiwe la msingi ili kuanza mchakato wa ujenzi wa uwanja huo, jambo ambalo hata aliyekuwa Mgeni Rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mama Fatuma Karume wamesifia kuwa ni kuonyesha kwa kiasi gani viongozi wa Yanga walivyo wasikivu na makini katika maamuzi.

Mwanaspoti linaamini zile ndoto za muda mrefu za wanachama wa Yanga kama ilivyo kwa wenzao wa Simba kuona klabu zao zinakuwa na viwanja vyao na kuepukana na gharama za kukodisha zinaanza kukaribia.

Simba na Yanga kwa muda mrefu zimekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuhama kutoka kiwanja kimoja hadi kingine ili kuwezesha vikosi vyao kufanya mazoezi, acha na kunyanyasika na viwanja vya kuchezea mechi zao za Ligi Kuu ama mashindano mengine.

Lakini wenzao Simba walikuwa wajanja baada ya kuwahi kununua eneo Bunju ambalo kwa sasa linaendelea vema kwa ajili ya kukamilisha awamu ya kwanza ya kupatikana kwa kiwanja cha mazoezi kwa ajili ya timu hiyo.

Ila kwa vile Yanga nao wamejikomboa ni wazi yale mapinduzi ya soka yaliyoonyeshwa na Azam inayomiliki uwanja wa kisasa na hosteli zake huko Chamazi, sasa yatahamia kwa klabu hizo kongwe za Simba na Yanga.

Kitu cha muhimu viongozi, wanachama na wadau wa klabu hizo washirikiane kuharakisha ujenzi wa viwanja hivyo na miradi mingine iliyokusudiwa kwenye maeneo ya ardhi za klabu hizo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa ubora zaidi.

Ilikuwa ni aibu kubwa kwa klabu zenye umri wa miaka 80 kushindwa kumiliki hata uwanja wa kufanyia mazoezi na kuachwa nyuma na klabu iliyozaliwa miaka 10 tu iliyopita, yaani Azam FC.

Tunaamini Simba na Yanga ni kiigizo kwa klabu nyingine nchini, lakini kuchelewa kwao kujiwezesha kimaendeleo ilikuwa ni kujidhalilisha mbele ya klabu nyingine ambazo ni ndogo. Ndio maana tunasema kwa hili la Yanga kufuata nyayo za watani zao ni ukomavu wa hali ya juu na kuthibitisha kuwa, klabu zetu kubwa zikiamua jambo zinaweza ila sema tu zinajichelewesha zenyewe kwa vile zina nguvu kubwa ya rasilimali watu.