Kuna mengi ya kujifunza kwa michuano hii ya klabu Afrika

MASHINDANO ya kimataifa siyo tu kusaka ushindi ndani ya uwanja, ni sehemu ya kujifunza wengine wanafanya kitu gani ambacho sisi hatufanyi.

Mashindano hayo ni fursa kubwa ya kufahamu wengine wamefanikiwa vipi na sisi tunakwama wapi. Ni fursa ya kipekee na ndiyo sababu tunategemea timu zinazoshiriki mashindano hayo ziwe tofauti na zile ambazo hazishiriki.

Ukiachana na matokeo waliyopata Yanga kwa kufungwa mabao 2-1 na Township Rollers ya Botswana huku Simba ikipata sare ya mabao 2-2 na Al Masry ya Misri, kuna vitu vingi vya kujifunza ndani na nje ya Uwanja.

Kwanza kabisa ni namna maandalizi ya mechi kubwa yanavyopaswa kufanyika. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeweka utaratibu mzuri katika mechi zake.

Kabla ya mchezo, Kamishna wa mechi husika hufanya ukaguzi wa kutosha kuona kama mchezo huo unaweza kufanyika. Kamishna huhakikisha kila utaratibu unaopaswa kufuatwa, umefuatwa.

Tunapaswa pia kuwa na utaratibu huu katika mashindano ya ndani. Tuache kufanya vitu kwa kukurupuka na badala yake turuhusu vitu vifanyike kwa weledi.

Kabla ya mechi, kuwe na watu wa kukagua mazingira kama yanaruhusu. Baadhi ya mechi zetu hazichezwi kwa utaratibu mzuri.

Kitu cha pili ni uwekezaji uliofanywa na timu za wenzetu uwanjani. Rollers na Al Masry walionekana kuwa na vikosi bora kuliko Simba na Yanga.

Timu hizo zilionekana kuwa na vikosi imara zaidi. Uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ulikuwa mkubwa kuliko ule wa wachezaji wa Simba na Yanga.

Mfano kwenye kikosi cha Al Masry straika wao matata, Aristide Bance alianzia benchi. Ni timu gani nchini inaweza kumuweka mchezaji mkali benchi?

Pia, timu za wenzetu zinaonekana kuwa na nidhamu kubwa ya mchezo. Makocha wa timu zao wanaonekana wazi kuwa wanapewa uhuru wa kufanya kazi yao.

Kitu cha tatu ni uwekezaji wa fedha kwenye soka. Rollers wanaweza kuwa funzo kubwa zaidi. Walionekana dhahiri kuwa wana fedha za kutosha. Tajiri wa timu hiyo naye alikuwa jukwaani kuongeza hamasa.

Uwekezaji huo ni kama ule uliofanywa na TP Mazembe. Mwaka 2011 Mazembe walipokuja kucheza na Simba hapa nchini, tajiri wao Moise Katumbi alikuwa jukwaa kuu kuongeza hamasa.

Ukiangalia kwa Tanzania, uwezekaji wa soka bado uko chini. Kuna wakati Yusuf Manji alikuwa akiisaidia Yanga lakini hakufikia kiwango cha Wabotswana hao.

Kwa sasa Mohammed Dewji ‘MO’ anaisaidia Simba lakini siyo kwa kiwango anachofanya Katumbi pale TP Mazembe ama cha Wabotswana hao.

Tunapenda kuzikumbusha timu zetu kwamba bado tuna vitu vingi vya kujifunza zaidi. Pia matajiri wanaosapoti soka wanapaswa kwenda uwanjani kutoa hamasa. Pesa siyo kila kitu, uwepo wao pia ni muhimu.

Wakati tajiri wa Township Rollers akisafiri kutoka Gaborone kuja nchini kuongeza hamasa kwa timu yake, MO hakuonekana kwenye mechi ya Simba na Al Masry. Kukosekana kwake inawezekana kwa kiasi fulani kupunguza hamasa kwa wachezaji.

Kitu kingine cha kujifunza ni namna wenzetu wanavyoichukulia michuana hiyo kwa uzito mkubwa. Timu zetu bado hazijaweza kuweka msisitizo mkubwa kwenye mashindano hayo.

Mfano wachezaji wa Township Rollers waliahidiwa posho ya Dola 5000 (Sh11 milioni) kwa kila mmoja endapo tu wangeifunga Yanga na wamefanikiwa. Hamasa yao ilikuwa juu.

Mabosi wa Rollers wanafahamu kwamba kwa kufuzu tu hatua ya makundi watapata zaidi ya Sh1.2 bilioni. Wanafahamu kwamba kadri wanavyoweka jina kubwa kwenye mashindano hayo, ndivyo watakavyopata wadhamini wengi zaidi.

Wanafahamu wazi kwamba kadri timu inavyosonga mbele ndivyo unavyotengeneza nafasi ya kuuza wachezaji wengi zaidi kwenda Ligi kubwa za Ulaya.

Kitu kingine cha kujifunza ni namna waamuzi wanapaswa kuwa na msimamo. Mwamuzi wa mechi ya Simba na Al Masry alitoa penalti tatu kwenye mchezo huo. Iliwashtua wengi. Kwa waamuzi wa Tanzania ni ngumu kutoa penalti nyingi kwenye mchezo mmoja. Pengine kwenye mchezo ule angeishia moja.