Yanga, Azam zimekosa mwendelezo wa kiwango

Muktasari:

Azam imeondolewa na Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 3-1, awali ilishinda hapa nyumbani bao 1-0, lakini ilipoenda kwenye marudiano huko ugenini ikachapwa 3-0.

KWA sasa, tayari moja ya timu mbili za soka zilizokuwa zinatuwakilisha katika mashindano ya klabu barani Afrika, Azam FC, imeshaondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kukwama katika raundi ya kwanza ilipoanzia.

Azam imeondolewa na Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 3-1, awali ilishinda hapa nyumbani bao 1-0, lakini ilipoenda kwenye marudiano huko ugenini ikachapwa 3-0.

Nyingine ni Yanga, imeondolea kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika lakini bado unapumua kiasi kwani kwa mfumo uliopo, imeangukia Kombe la Shirikisho lakini uhai wake utaonekana tu kama itashinda mechi ya mtoano inayoikabili dhidi ya waarabu MC Alger ya Algeria.

Yanga ilikwama mbele ya Zanaco ya Zambia iliyopenya kwa faida ya bao la ugenini, awali jijini Dar zilifungana 1-1 lakini kwenye marudiano jijini Lusaka hakuna aliyeweza kuliona lango la mwenzake.

Kwa miaka takriban minne mfululizo, timu hizi mbili zimekuwa zikipata nafasi kwa pamoja ya kutuwakilisha katika michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu kutokana na kufanya kwao vizuri katika ligi ya nyumbani.

Lakini bahati mbaya timu zote hizo zimekosa mwendelezo unaoshawishi.

Yanga kwa uzoefu ilionao wa kushiriki katika mashindano hayo kwa miaka mingi, inatosha kabisa kuwa deni. Kama kujifunza ina uzoefu wa kutosha.

Kwa Azam inawezekana kabisa kushindwa kwao msimu huu pia kukawa na sababu ya kuendelea kujifunza kutokana na ugeni wao katika mashindano haya kwani hata huo ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza waliupata mwaka 2014, yaani miaka mitatu tu iliyopita.

Kabla ya hapo waliwahi kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho pale waliposhika nafasa ya pili kwenye ligi ya msimu 2013/2014, walipotia mguu wakatolewa katika hatua ya awali na Ferroviario da Beira ya Msumbiji.

Na walitolewa hivi hivi kwa kushinda bao moja nyumbani kisha kufungwa 2-0 ugenini. Mwaka 2015 walishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kuondolewa pia katika hatua ya awali na El Merreikh ya Sudan kwa kushinda 2-0 nyumbani kisha kuchapwa 3-0 ugenini.

Msimu uliopita Azam ilionekana kuimarika kwani ilifanikiwa kuiondoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini pale ilipoifunga katika mechi ya kwanza ugenini 3-0 na kuifunga tena nyumbani 4-3, lakini ikaondolewa katika hatua ya pili na Esperance ya Tunisia. Nyumbani Azam ilitamba 2-1 lakini ugenini ikalala 3-0.

Ukiyaangalia matokeo hayo ya Azam unaweza kuona kabisa kuwa msimu huu timu hiyo ilitakiwa kusogea mbele zaidi ya pale ilipofikia msimu uliopita.

Yanga nayo ambayo ina historia ndefu ingawa historia yenyewe ni ile ya kushiriki na kutokufanikiwa katika michuano ya kimitaifa, ilitakiwa pia kusogea mbele zaidi.

Msimu uliopita pia walidondokea Kombe la Shirikisho kama hivi ambapo walikutana na Sagrada Esperanca ya Angola, Yanga ikashinda 2-0 kwenye mechi ya kwanza hapa nyumbani, ikafungwa 1-0 kwenye mechi ya pili ya ugenini hivyo kuingia katika hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa 2-1. Lakini huku kwenye makundi ilishinda mechi moja tu na kupata sare moja kati ya michezo sita, ikafia hapo.

Ili mwendelezo uonekane kuwepo kwa timu ya Yanga kutoka katika msimu uliopita, ilitakiwa msimu huu timu iingie katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa au sasa iingie makundi ya Kombe la Shirikisho na ihakikishe inafika hatua ya nusu fainali.

Bahati mbaya kwa timu hizi zote mbili ni kuwa zimekosa mwendelezo kwa kuwa hazikuwa na mpango kazi unaoziongoza kufikia katika malengo.

Kama zingekuwa na mpango kazi zisingeingia katika hatua hii bila ya kuwa na vikosi imara zaidi.