MTAA WA KATI : Wenger asipobadilika, atabadilishwa tu

Muktasari:

  • Arsenal ni ile ile, hakuna budi wenye kuipenda na kuishangalia waendelee tu kufanya hivyo. Hakuna namna, labda kama Arsene Wenger ataamka na ubavu mwingine si ule wa kila siku.

MABADILIKO. Huu ni msamiati mgumu sana Arsenal. Ndiyo, usinibishie. Msimu mpya wa Ligi Kuu England umeanza, lakini matatizo ya Arsenal ni yale yale ya miaka yote.

Arsenal ni ile ile, hakuna budi wenye kuipenda na kuishangalia waendelee tu kufanya hivyo. Hakuna namna, labda kama Arsene Wenger ataamka na ubavu mwingine si ule wa kila siku.

Alipofanya usajili ule wa Granit Xhaka, tena kwa pesa nyingi. Pauni 35 milioni mapema tu mwanzoni mwa majira ya kiangazi, mashabiki wa timu yake waliamini kwamba msimu huu utakuwa na mabadiliko. Kocha wao atakuwa amejifunza kutokana na kile kilichotokea kwa miaka 12 timu hiyo. Na wakati huu akiwa kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake, atataka awaache mashabiki na kitu cha kujivunia, taji la Ligi Kuu England.

Kufumba na kufumbua, msimu mpya umeanza. Waliongezeka baada ya Xhaka ni Rob Holding na Asano Takuma. Yaani beki wa Pauni 2.5 milioni na straika kinda wa Kijapani. Wenger anautani, anawatania mashabiki wa Arsenal, ambao ndiyo hasa wanaoumia kwa matokeo ya timu yao.

Agosti 31 usajili wa majira haya ya kiangazi utafungwa rasmi. Utafunguliwa tena Januari mwakani, kipindi ambacho usipojipanga vizuri kwa sasa, wakati huo utakuwa unapambana tu ama ubaki kwenye ligi usishuke, au kupambana walau ufuzu kucheza moja ya michuano hii miwili ya Ulaya, Ligi ya Mabingwa Ulaya au Europa League.

Ni muda sasa tangu zisikike stori kwamba Wenger anataka kusajili straika wa nguvu. Anataka kusajili beki wa nguvu. Wenzake wamefanya usajili mapema, ili ikapofika Septemba wakati ligi imeshangaza, wachezaji wanaokuwa wameelewana vyema. Lakini, Wenger anasubiri kusajili mkesha wa kuamkia Septemba Mosi, hadi wachezaji wake wapya waanze kuelewana na wenzao ishafika Oktoba au Novemba. Kidogo tu, Desemba hiyo, stori inaendelea kuwa ileile. Stori za sasa za usajili zinazomhusu Wenger ni straika wa Lyon, Alexandre Lacazette na beki wa Valencia, Skhodran Mustafi. Lakini, wiki zinakatika sasa, hakuna cha Lacazette wala Mustafi. Inasemekana dili la Mustafi linachelewa kukamilika hadi sasa kwa sababu Wenger na Valencia wanabishania pesa ndogo sana, Mfaransa huyo anasuasua kulipa. Pesa kiduchu sana, lakini Wenger anaona kama analiwa vile. Jumapili, wakati anapigwa 4-3 na Liverpool kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu, huko Ufaransa Lacazette alipiga ‘hat-trick’ kwenye mechi ya kwanza ya Ligue 1 akiwa na Lyon. Unadhani Lacazette atapatikana kwa bei rahisi tena?

Kipigo kutoka kwa Liverpool kina madhara makubwa kwa Wenger. Kwa sasa hana ujanja zaidi ya kusajili tu, hasa kwa wachezaji wa safu ya ulinzi na ushambuliaji. Hiki ni kipindi cha kupigwa pesa sasa, kwa sababu watakaomuuzia wanafahamu wazi ni lazima anunue, la basi asubiri majanga ya kuzomewa tu na mashabiki wake kwa msimu wote.

Mabadiliko wanayoyataka mashabiki wa Arsenal kasi yake ni tofauti na anavyotaka kocha wao. Juzi alianza ligi kwa kupanga mabeki wa kati dhaifu sana. Holding na Calum Chambers. Hawakumweza kabisa Sadio Mane. Hawakumweza Philippe Coutinho na hata Adam Lallana.