Wachezaji waitumie vyema likizo ya Ligi Kuu

Muktasari:

  • Wapo waliofanya vyema kwenye duru la kwanza ni wajibu wao kuhakikisha ubora na viwango vyao unabaki kama ulivyo ama unaongezeka zaidi kwa duru lijalo, kadhalika wale waliochemsha wajipange tena ili warudi kivingine.

KLABU 16 za Ligi Kuu Bara na nyingine 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zipo mapumziko baada ya kumalizika kwa mechi za duru la kwanza.

Kwa wachezaji na makocha ni nafasi yao ya kujitathmini katika kipindi hiki, sambamba na kutumia likizo hiyo fupi kupumzisha miili na akili zao baada ya mikikimikiki.

Ni fursa nzuri kutokana na ukweli kuwa ndio wanaovuja jasho uwanjani, hivyo ni wajibu wao kutumia mapumziko haya kutuliza miili na akili zao ili duru lijalo warejee wakiwa kama wamezaliwa upya katika kuzipigania timu zao.

Wapo waliofanya vyema kwenye duru la kwanza ni wajibu wao kuhakikisha ubora na viwango vyao unabaki kama ulivyo ama unaongezeka zaidi kwa duru lijalo, kadhalika wale waliochemsha wajipange tena ili warudi kivingine.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya ni kuwa wapo baadhi ya wachezaji kipindi hiki cha mapumziko, ndio kama wamepewa uhuru wa kujirusha watakavyo, kujigeuza Popo kwa kukesha kwenye kumbi za burudani na kuchati na rafiki ama wapenzi wao mpaka alfajiri bila kujua kama wanazidi kuichosha miili yao kuliko ligi ilipokuwa ikichezwa.

Baadhi ya wachezaji wakati kama huu ndipo watakokimbilia kucheza mechi za ndondo kwa ajili ya kuganga njaa, bila kujali athari inayowakabili kama wakiumia huko mchangani na wengine hula na kunywa chochote kama vile wamestaafu sasa wanajiachia tu kwa kuwa hakuna wa kuwafuatilia kama inavyokuwa wanapokuwa kambini.

Mwanaspoti linawakumbusha kuwa, soka ni ajira hivyo kufanya jambo ambalo litawaharibia soka lao, maana yake ni kujiharibia mustakabali wa maisha yao kwa jumla. Kwa misimu kadhaa tumekuwa tukishuhudia baadhi ya klabu na wachezaji wamekuwa wakifanya vyema kwenye duru la kwanza, lakini pale duru la pili linapoanza huyumba kiasi cha kushangaza. Baadhi ya wachezaji hurudi wakiwa wazito kutokana na kujiachia sana, kiasi cha kuifanya miili yao itutumke mno. Hii yote inatokana na wachezaji kushindwa kutumia vyema mapumziko yao kujitathimini na kujiweka fiti kwa duru la lala salama, ndiyo maana kama wadau wa soka tunawakumbusha wachezaji wasifanye makosa tena.

Ndiyo maana tunasisitiza kuwa, wachezaji lazima watumie mapumziko yao vyema kama ambavyo makocha, waamuzi na hata mabosi wa klabu shiriki za Ligi Kuu na ile ya FDL kujitathimini na kurekebisha walipoteleza ili duru lijalo linoge zaidi.