Waamuzi wasilivuruge pambano la watani

Friday February 24 2017Mashabiki wa Klabu za Yanga na Simba

Mashabiki wa Klabu za Yanga na Simba 

By MWANASPOTI

ZIMESALIA saa chache kabla ya watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga kuvaana katika pambano la marudiano la Ligi Kuu Bara msimu huu.

Timu hizo zitapepetana kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika pambano lao la 98 tangu kuasisiwa kwa Ligi ya soka Tanzania Bara mnamo mwaka 1965.

Tayari viongozi, wachezaji, makocha, mashabiki na wanachama wa klabu hizo wameanza kutambiana kila upande ukitamba kuibuka na ushindi japo ukweli matokeo katika soka ni baada ya dakika 90.

Mitaani ni tambo, kejeli na amsha amsha zinazohamasisha pambano hilo kubwa miongoni mwa mapambano ya watani na wapinzani wa jadi barani Afrika.

Hii yote ni kuonyesha namna gani pambano hilo linavyochukuliwa kwa uzito mkubwa miongoni mwa Watanzania ambao soka ni mchezo wanaoupenda.

Katika Ligi Kuu kuna mechi zaidi ya 200, lakini kila linapokuja pambano la watani hali huwa tofauti kutokana na ukweli huwa ni la kipekee na lenye mvuto wa aina yake na kuteka hisia za wengi wakiwamo hata viongozi na wanasiasa.

Katika kuonyesha kuwa pambano hili la marudiano linachukuliwa kwa uzito mkubwa mpaka asubuhi ya jana Alhamisi jina la mwamuzi wa kulichezesha pambano hilo halikuwa likifahamika kutokana na kufanywa siri.

Hii ni tofauti na mapambano mengine ambayo waamuzi hufahamika kulingana na ratiba yao na hata linapokuja pambano la Simba na Yanga hutajwa wiki moja kabla, lakini safari hii limefichwa kwa kile kilichoelezwa kuhofia asirubuniwe.

Ni wazi kumbe waamuzi wamekuwa wakirubuniwa na baadhi ya klabu na wakati mwingine kuingia uwanjani kuchezesha mechi za Ligi Kuu na hata zile za Ligi Daraja la Kwanza na Pili wakiwa na matokeo yao kichwani. Hii ni hatari.

Katika mechi iliyopita iliyochezwa Oktoba Mosi, mwaka jana pambano la watani nusura livurugike baada ya Simba kupinga bao la Amissi Tambwe wa Yanga na kusababisha mashabiki wao kuvunja na kung’oa viti.

Ndani ya uwanja wachezaji walimpa kashkashi Mwamuzi, Martin Saanya kiasi cha kuanguka chini na kumlima kadi nyekundu nahodha wa Simba, Jonas Mkude kabla ya TFF kuingilia kati na kuifuta kadi hiyo haraka, huku Saanya akisimamishwa.

Mwanaspoti linafahamu kuwa ni lazima pambano hilo la kesho lichezeshwe na waamuzi wale wale waliozoeleka katika ligi yetu. Hawatatoka nje ya nchi kama Simba ilivyokuwa ikililia kipindi fulani na bahati nzuri serikali na TFF imechimba mkwara kwa mashabiki juu ya kuwa makini na kutojihusisha na vurugu kesho.

Lakini tuna wito kwa waamuzi watakaopangwa ama waliopangwa kuichezesha pambano hilo kuwa ni lazima watende haki na kutimiza wajibu wao kwa kutumia sehria 17 za soka pamoja na busara na hekima ili mchezo uishe salama.

Maamuzi mabovu na yenye kuongozwa na hisia, ushabiki ama shinikizo ni hatari na yanaweza kulivuruga pambano hilo na kusababisha vurugu zisizo za lazima.

Hivyo, waamuzi watakaolichezesha wafanye kazi yao kwa weledi, uadilifu na uaminifu kwa kuwaacha wachezaji wapambane wenyewe kusaka matokeo na mwishowe mshindi apatikane kihalali.

Kulichezesha vema pambano hilo sio tu watakuwa wanazitendea haki timu zote, lakini pia watakuwa wanalijengea heshima soka la Tanzania na pia kujitangaza na kujijengea heshima wao binafsi.

Pambano la Simba na Yanga linafuatiliwa na kuangaliwa na mashabiki wa ndani na nje ya nchi, hivyo lolote baya watakalofanya waamuzi kulivuruga watajiharibia wenyewe na pia kutoa taswira mbaya ya soka la Tanzania.

Ndio maana tunawasisitiza na kuwaomba waamuzi wa pambano la la kesho kutenda haki na kusaidia kuwaepushia kazi za ziada askari watakaokuwa wakilinda usalama uwanjani hapo kwa kutowachochea mashabiki wafanye fujo.