Tanzania tukijipanga tutaenda Cameroon

Muktasari:

  • Tusidanganye. Kundi hilo sio jepesi hata kidogo, japo sio gumu kama ilivyokuwa misimu mfululizo iliyopita ambapo Tanzania ilikuwa ikiwekwa sambamba na vigogo kiasi cha kuikatisha tamaa kabla hata haijaanza kushiriki mbio hizo.

 SHIRIKISHO la Soka Afrika (Caf), mwishoni mwa wiki iliyopita lilitangaza makundi ya michuano ya kuwania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa mwaka 2019.

Michuano hiyo ijayo itafanyika nchini Cameroon na katika namna ya kustaajabisha kabisa Tanzania safari hii ikajikuta kwenye kundi ambalo sio gumu wala sio jepesi, kitu ambacho ni muda mrefu kufanyiwa hivyo.

Katika kundi lao Tanzania imepangwa na mataifa ya Uganda, Cape Verde na Lesotho wakiwekwa Kundi L ambalo ni la mwisho kabisa katika orodha ya makundi ya michuano ya fainali hizo za 2019.

Mara baada ya droo hiyo, baadhi ya mashabiki wa soka wamekuwa wakitoa maoni yao wakiamini kuwa Tanzania imepangwa kundi mchekea na wapo walioikatia tamaa Taifa Stars kutokana na rekodi zao katika mechi za karibuni. Tusidanganye. Kundi hilo sio jepesi hata kidogo, japo sio gumu kama ilivyokuwa misimu mfululizo iliyopita ambapo Tanzania ilikuwa ikiwekwa sambamba na vigogo kiasi cha kuikatisha tamaa kabla hata haijaanza kushiriki mbio hizo.

Uganda sio timu nyepesi hata kidogo na ndio maana ipo Gabon ikishiriki fainali za Afcon za mwaka huu, Cape Verde nao sio ya kubezwa kwani kwa miaka ya karibuni imeonekana kuimarika zaidi kiasi cha kuweza kushiriki fainali mbili mfululizo za Afcon, 2013 na 2015.

Nchi hiyo iliyopata uhuru mwaka 1975 tuliwahi kupangwa nao kwenye mbio za kuwania fainali za Afcon 2010 na Kombe la Dunia la mwaka huo lililofanyika Afrika Kusini, ambapo walitufungwa kwao bao 1-0 na tukalipa kisasi kwa 3-1.

Katika kundi letu tulipangwa na Cameroon na Mauritus na Cape Verde walimaliza nafasi ya pili juu yetu na tangu hapo hatujawahi kuwakamata tena kwani wamekuwa wakisonga kila uchao. Lesotho nao si wepesi kwani ni hivi karibuni walituzabua kwenye michuano ya Cosafa tuliyoalikwa kuonyesha kuwa ni lazima tujipange kwelikweli kama tunataka kwenda Cameroon.

Hatupaswi kuikatia tamaa Tanzania, lakini tusijipe moyo na kujiaminisha kuwa tutapenya kirahisi kwenye kundi hilo, hata kama hakuna vigogo. Uganda kwa sasa wametuacha mbali na wamekuwa wakitukwamisha mara kadhaa.

Mwanaspoti linadhani ni wakati wa serikali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau wengine kuanza kampeni ya mapema ili kuiwezesha Tanzania kufanya vema kwenye mechi zao za kundi hilo ili kurejea mafanikio ya mwaka 1980.

Mwaka huo Tanzania ilienda Afcon zilizofanyika nchini Nigeria na tangu hapo imekuwa ikihaha kwa miaka zaidi ya 35 sasa ikisaka tiketi za kwenda katika fainali hizo. Caf safari hii ni kama wametupendelea, kwani hatujaanzia hatua ya awali, tumeingia moja kwa moja kwenye makundi, tunataka nini tena kama sio kuanza maandalizi mapema na kuhakikisha wachezaji wetu wanaandaliwa kisaikolojia ili kupambana kiume na kufuzu fainali hizo zijazo za Cameroon.

Tunaamini Tanzania imejaliwa vipaji vingi, ina hazina kubwa ya makocha na hata wadau wenye mapenzi makubwa ya michezo hususani soka, kwanini sasa kwa umoja wetu tusiunganishe nguvu na kuanzisha kampeni itakayotupeleka Afcon?

Tusikae tukisubiri miujiza ama watu kujitokeza mwishoni wakati imesalia mechi moja ama mbili na kuwatia wazimu wachezaji wetu kwa ahadi za mamilioni, wakati kipindi cha maandalizi tunaitelekeza timu na kuwakatisha tamaa kabisa.