MSINIBISHIE : Serengeti Boys inahitaji msaada zaidi siyo sifa

Saturday February 11 2017JULIUS KIHAMPA

JULIUS KIHAMPA 

By Julius Kihampa

TIMU ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imepata nafasi ya kucheza fainali za vijana za Afrika baada ya kufanikiwa kushinda rufani yake.

Serengeti Boys ilimkatia rufani mchezaji wa Congo-Brazzaville, Langa Lesse Bercy aliyedaiwa kuwa na umri zaidi ya unaotakiwa kwa michuano hiyo.

Kwa matokeo hayo, vijana wetu sasa watacheza wakiwa Kundi B, lenye timu za Angola, Mabingwa watetezi Mali na Niger.

Mashindano hayo msimu huu yamepangwa kufanyika Gabon, ambako zilifanyika fainali za Afcon 2017, wakati Cameroon ikitwaa ubingwa.

Umekuwa wakati mzuri kwa Kocha, Bakar Shime kuandaa kikosi na kila mdau wa soka nchini anaonekana kufurahia mafanikio hayo ya vijana.

Bila kuwa wanafiki, tungependa zaidi kikosi cha wakubwa, Taifa Stars kingefuzu kwa fainali za Afcon, lakini hatukuwahi kucheza tangu tulipofanya hivyo mara ya mwisho 1980.

Lakini kwa sababu vijana wetu wamepata nafasi hiyo, hatuna budi kuwa nyuma yao kuonyesha kwamba tunaunga mkono jitihada zao kwa ajili ya timu ijayo ya Taifa Stars.

Wasiwasi wangu tu katika hili kama tutaanza kuingiza siasa mapema katika maandalizi ya vijana hawa bila kujua tunakwenda kucheza mashindano yenye ukubwa gani.

Wakati mwingine tunakuwa kama tumerogwa tunapoona kuna nafasi kama hii ya kucheza katika mashindano makubwa na hapo ndipo kila mtu anataka kuonekana wa muhimu.

Juzi vijana wetu walianza kwa kupata mwaliko bungeni, jambo la kheri lakini wanahitaji zaidi ya kuonekana katika runinga wakiwa na wabunge.

Bajeti yao inaonyesha kuwa imefika zaidi ya Sh1 bilioni hadi kumaliza wiki mbili za mashindano hayo nchini Gabon.

Huu sasa ndiyo wakati wa kuonyesha kuwa sote tupo katika mapambano ya mafanikio wanayoyatafuta Serengeti badala ya kuwaingizia siasa ambazo haziwezi kuwasaidia mashindanoni.

Tunachoshindwa sisi ni pale kila mtu anapotaka kuonekana ana umuhimu wakati suala limeshakamilika kama ilivyo kwa vijana hawa.

Wamepambana bila kuwa na udhamini wa kueleweka, tunatakiwa basi tuongeze morali yao kwa ukweli na si kufanya kuonekana kutokana na walipofikia.

Serikali za wenzetu zina mchango mkubwa katika suala kama hili la mafanikio, nadhani nasi tunaweza kuliiga hilo kwa chochote na hata kusaidia kuwapigia debe kupata fedha zaidi.

Serikali kupitia kwa Wizara ya Habari, Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo inaweza kabisa kutumia cheo chake kuzungumza na wadau katika kampeni ya kutafuta Sh1 bilioni kwa ajili ya ushiriki wao.

Wasiwasi wangu tutaendelea na mazoea yetu tukisubiri watolewe kipuuzi na kuanza kuwalaumu wakati tulikuwa na uwezo wa kuwasaidia kabla.

Hatuna sababu ya msingi ya kulikimbia hili, hawa ni vijana wetu na bila ubishi tunatakiwa kutoa sapoti ya kweli badala ya kutafuta sifa katika migongo yao.