MEZA YA UFUNDI : Ratiba inazinyima timu ndogo kuleta ushindani

Saturday February 11 2017Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By Joseph Kanakamfumu kanakamfumujoseph @yahoo.com

HAKUNA mpenda michezo nchini hasa soka asiyependa ushindani kwenye michezo ya michuano mbalimbali inayoendelea. Mpenzi na shabiki wa kweli wa soka atatamani kila timu iwe inapoteza mchezo ndani na nje ya mkoa wake.

Mpenzi wa kweli wa soka la Tanzania bila kujali itikadi za kiushabiki za ama Yanga au Simba atataka timu zote kubwa zisiwe zikipata ushindi kirahisi tu zinapotoka nje ya Dar es Salaam zinahitajika kutoa jasho badala ya kushinda kirahisi.

Lakini wadau wa soka nchini wanahitaji kuuona ushindani huo ukiwa ‘fair’ si wa kulazimisha hivyo ukimpata Simba ama Yanga mkoani mfunge na si kumuonea huruma ya kishabiki.

Bado timu hizo nyingi zikiwa ni za mikoani na chache za Dar es Salaam zinatakiwa ziwe na vyanzo mbadala vya pesa zitakazowawezesha kuingia kwenye ushindani wa kweli na timu za Azam, Simba na Yanga.

Hii itazifanya ziwe na uwezo wa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu iwe ni wa ndani ama nje ya nchi, zikiwa pia na uwezo wa kuwalipa vizuri wachezaji wao ili kuamsha ari kubwa ya upiganaji wa kupata matokeo mazuri.

Kadhalika na kucheza soka zuri la ushindani ndani ya uwanja bila shaka hili ndilo linalotakiwa kuwa.

Majibu ya ushindani huu yataonekana pale timu zetu zinazopata uwakilishi kimataifa zitakapoweza kucheza kwa ushindani mkubwa na kupata matokeo mazuri uwanjani.

Lakini bado timu zetu tunazoziita ndogo kwa sababu ya mafanikio asiyoyapata ndani ya ligi kuu kwa muda mrefu wa ushiriki wao na pia kutokuwa na nguvu nzuri ya kiuchumi ukilinganisha na Azam, Simba na Yanga ambazo zina nguvu kubwa ya kiuchumi na tayari zina mafanikio kiasi kimataifa.

Ukilinganisha na hawa wengine naisema Azam pamoja na Simba na Yanga kwa kuwa tayari Azam ameshapata mafanikio ndani ya ligi yetu ikiwa imechukua ubingwa huo mara moja sawa na timu nyingine za zamani kama Coastal Union, Tukuyu Stars, Pan, Mseto na Cosmo pia ikiwa imeshashinda ubingwa wa Afrika Mashariki na kushinda michuano mingine mingi tu ya ndani ya Tanzania.

Timu hizi ndogo bado zinapigana kwanza kuleta ushindani ndani ya ligi lakini hazifanikiwi hivyo kuziacha kila mwaka klabu kubwa zikifanikiwa kuchukua nafasi mbili za juu kuiwakilisha nchi yetu ya Tanzania kila mara.

Ni kweli timu hizi hazileti ushindani mkubwa mbele ya timu hizo tatu ikiwa ni nje ya uwezo wao!

Sasa badala ya kuzisaidia klabu hizi hata pale kwenye uwezekano wa kusaidiwa bado TFF na Bodi ya Ligi kupitia sehemu nyingine wanazifanya klabu hizo kuwa na wakati mgumu wa kutoa upinzani mbele ya timu hizo.

Moja ya tatizo kubwa wanalolipata wadogo hao ni pale unapoona timu moja inapangiwa ratiba ngumu kuelekea mchezo unaozihusu timu mojawapo.

Huko nyuma ilitokea pale Kagera Sugar ilipokuwa inatakiwa kucheza na Yanga Jumamosi Kaitaba ikiwa imetoka kucheza mechi Mlandizi, Pwani Jumanne na kulazimika kusafiri siku mbili ikiwa njiani na kuikuta Yanga ilishafika zamani baada ya kucheza Mwanza Jumatano kwa nini isifungwe?

Leo hii ndani ya dimba la Taifa kutakuwa na mchezo baina ya Simba na Prisons ambayo imecheza mjini Mbeya Jumatano dhidi ya JKT Ruvu, hivyo kusafiri siku nzima ya Alhamisi ikiwa imepumzika kidogo jana na hivi leo tunaiona Taifa.

Simba ilikcheza mchezo wao Jumamosi iliyopita mjini Songea na kurudi Jumapili na kupumzika bila shaka imefanya mazoezi Jumanne hadi jana ikiwa haina uchovu wowote ule hapo kwa mwenye akili anaona kila kitu. Mambo yapo wazi kabisa.

Lengo la waliopanga ratiba hii ni kuhakikisha Prisons inakosa nguvu zake zote ilizokuwa nazo na hivyo kuwa rahisi kwao kupoteza mchezo wa leo!

Sitegemei kuiona Simba ikipata upinzani mkubwa kama ilivyoupata kule Mbeya ilipopoteza kwa goli 2-1, labda tu iwe ni ubishi na uwezo wa kujituma kwa wachezaji wa Prisons ndio unaoweza kuleta upinzani utakaotoa matokeo hasi kwa Simba.