Okwi akirudi Simba, Ulimwengu Yanga basi tatizo ni kubwa

Muktasari:

Habari ya Okwi nikaona kama ngumu. Hali ya kiuchumi ya Simba sio nzuri. Lakini kama ingekuwa nzuri, halafu Okwi mwenyewe akataka, halafu timu yake anayochezea Denmark ikaridhia, basi hilo ni dili linalowezekana kabisa.

HUWA nasikia katika mazungumzo ya baa. Nasikia kwamba Emmanuel Okwi anarudi Simba. Halafu nikasikia kwamba Yanga inamfukuzia Thomas Ulimwengu ambaye mkataba wake na TP Mazembe ulikata roho na sasa yupo huru. Wazungu wanamuita Free Agent.

Habari ya Okwi nikaona kama ngumu. Hali ya kiuchumi ya Simba sio nzuri. Lakini kama ingekuwa nzuri, halafu Okwi mwenyewe akataka, halafu timu yake anayochezea Denmark ikaridhia, basi hilo ni dili linalowezekana kabisa.

Na huku kwa Ulimwengu niliona sio kweli. Ulimwengu ninayemfahamu, jinsi alivyoacha pesa nyingi katika mkataba wake mpya ambao angeweza kuusaini, anawezaje kwenda Yanga. Yanga inaweza kumlipa zaidi ya Dola 15,000 kwa Mwezi? Wanachama si watataka afunge mabao mawili kila mechi?

Katika hali halisi kama haya yote mawili kwa mfano yakatokea, basi ujue soka letu lipo katika matatizo makubwa sana. Halitakuwa jambo la kushangilia kama mashabiki wanavyoshangilia kimya kimya na vyombo vya habari vinavyojaribu kuombea iwe kweli.

Unaanza na Okwi kwanza. Yule Okwi wa miaka mitatu nyuma alikuwa akikonga nyoyo za mashabiki wote wa soka Tanzania. Wale wa Simba walikuwa wanapagawa hadharani, wale wa Yanga walikuwa wanasonya hadharani halafu wanamkubali kimya kimya.

Ingawa Okwi ni Mganda na wala asingeweza kuisaidia Taifa Stars lakini wote tulikuwa tunajiuliza swali moja tu, Hivi Okwi anashindwa nini kucheza Ulaya? Ukweli ni kwamba alikuwa ana kila kitu. Na sasa kama Okwi akirudia Simba atazua maswali mengi zaidi na kuua morali ya wachezaji wengi chipukizi nchini.

Baadhi ya makinda wetu wataanza kuona Ulaya ni ngumu. Watabakiwa na mfano pekee wa Mbwana Samatta. Wengi wetu tulikuwa tunatabiri kwamba Okwi ataishia katika anga za Borussia Dortmund, Napoli, Tottenham na kwingineko. Vijana wetu watajiuliza, kama Okwi kashindwa na amerudi Simba, nani ataweza?

Lakini pili tutaanza kujiuliza ubora wa ligi yetu. Ina maana ligi yetu imefikia hatua ya kwamba mchezaji anaweza kuwa staa wa kiwango cha Okwi halafu akashindwa kufanikiwa Ulaya? Hili nalo litaua morali kuwa kumbe ligi yetu haimuandai mchezaji kucheza Ulaya.

Huku upande wa Ulimwengu ndio utanyong’onyesha wengi sana. Afadhali nasikia mwenyewe amekanusha. Jaribu kujiuliza, kama Thomas anarudi Bongo badala ya kumfuata Samatta nani atamfuata Samatta sasa?

Kwa ule mwili wake, kasi yake, nguvu zake, nani atacheza Ulaya kama Thomas atashindwa? Kuna mchezaji mmoja tu ambaye anafuata nyayo za Samatta kwa ukaribu, naye ni Thomas, kama Thomas haendi nani sasa ataenda? Unaweza kumsamahe kidogo Farid Mussa kwa chochote kinachomtokea kwa sasa, lakini unawezaje kumsamehe Thomas Ulimwengu?

Ukimfikiria Thomas ndipo unajuliza maswali mengi zaidi. Baada ya kucheza TP Mazembe na kufaidi pesa, kuendesha magari ya kifahari, kujenga nyumba za kifahari, kucheza mechi za klabu bingwa ya dunia, kuchukua ubingwa wa Afrika, unawezaje kurudi Dar es salaam na kucheza Yanga?

Ukifikiria hilo roho inakuuma ingawa Thomas sio ndugu yako wa tumbo moja. Hata hivyo, unabakisha akiba ya maneno kwa sababu kuna wachezaji wengi wametuangusha huko nyuma. Kuna wachezaji tuliwaamini, tukadhani wana akili nyingi, tukadhani wana vipaji vikubwa vya kucheza mbali, lakini mwishowe walisababisha tufiche sura zetu.

Hata hivyo, ikitokea hii ya Thomas basi nadhani kutakuwa na umuhimu wa kuendesha zoezi la upimwaji wa akili kwa wanasoka wote wa Tanzania ndani na nje ya mipaka yetu.

Itakuwa ni lazima kuwapima wachezaji wote nchini hasa wale wa nyumbani kabla hawajagusa uwanja wa soka.

Hivi vitu sio vya kushangilia sana wakati mwingine. Hivi ndivyo vinarudisha nyuma soka letu na kuua morali ya wachezaji chipukizi nchini kote.

Wenzetu wamefanikiwa kwa sababu walisoma historia ya mashujaa wao ‘Role Models’ na kufuata nyayo zao.

Kama Okwi anarudi Simba, au Ulimwengu anakwenda Yanga unajiuliza watoto wadogo ambao wamekuwa wakijitokeza katika Uwanja wa Taifa au wakisimama mbele ya runinga za majumbani kwao wataiga nini zaidi kutoka kwao kwa ajili ya kupata mafanikio na kufikia viwango vya kina Sadio Mane?