Nyasi bandia za Simba na blah blah tu

Saturday April 1 2017

 

By Angetile Osiah

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, ametangaza kuwa klabu hiyo imeshapata fedha za kukombolea nyasi bandia kwa ajili ya uwanja wao wa mazoezi, hivyo kuhitimisha mjadala wa takribani siku tano kuhusu vifaa vya michezo kutozwa kodi.

Nimekuwa nikifuatilia mjadala huo tangu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipotangaza kusudio la kuzipiga mnada nyasi hizo kutokana na muda wake wa kulipiwa ushuru kuisha na hivyo kuingia katika kipindi kingine cha siku 30 kusubiri kupigwa mnada.

Hoja za wengi zimekuwa ni kuisihi serikali iisamehe Simba na pia kutangaza kuondoa kodi katika vifaa vya michezo ‘ili ionyeshe mchango wake katika kuendeleza michezo’.

Hoja hizo zimekuwa zikitiwa nguvu na mifano mingi ya jinsi michezo ilivyokuwa ikiendeshwa huko nyuma, ambapo vifaa vya michezo vilikuwa vikimwagwa mashuleni na vyuoni na watoto kucheza wanavyotaka.

Wanadai bila ya serikali kutia mkono wake katika kuondoa kodi, michezo itaendelea kuwa nyuma. Kibaya zaidi hoja hizo zinatiwa nguvu na mifano ya kejeli kwa serikali kuwa ushiriki wake katika michezo umekuwa ni ‘katika kuaga timu za Taifa kwa kuzikabidhi bendera, kufungua na kufunga mashindano’.

Bahati mbaya sana maisha ni katili. Maisha hayatupi nafasi ya kurudi nyuma na kurekebisha, kufuta makosa au kurudia enzi bora maishani. Bali maisha yanatupa nafasi ya kuangalia nyuma na kujisahihisha ili tusirudie makosa tuliyofanya huko nyuma.

Kwa hiyo, hatuwezi kurejesha enzi za akina Leodegar Tenga waliokuwa wakisoma Chuo Kikuu huku wakisakata soka, au akina Sunday Manara, Adolph Rishard, George Kulagwa au Willy Mwaijibe.

Bali maisha yanatupa nafasi ya kuangalia walifanya nini, walipatia wapi na walikosea wapi ili tujifunze kutokana na mazuri au mabaya yao tuweze kukabiliana na hali ya sasa ambayo ni tofauti kabisa na mazingira ya hao wakongwe wetu.

Ukirejea kipindi hicho, ni dhahiri kuwa soka lilikuwa la ridhaa, siasa duniani zilikuwa za vita baridi zilizotufanya tuweze kupata misaada kutoka upande mmoja wa vita hiyo, michezo haikuwa biashara kubwa kama ilivyo sasa na pia nchi zetu ndio kwanza zilikuwa zimetoka kupata uhuru, hivyo serikali zilikuwa zikiangalia jinsi ya kusaidia kila nyanja ili ikifikia wakati fulani kila sehemu isimame peke yake na kujitegemea.

Hizo ndizo enzi ambazo shule ziliweza kupata vifaa vya michezo, mashindano yaliweza kufanyika kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, walimu waliweza kufundishwa ualimu wa michezo na wengine kwenda hadi nchi za Romania, Hungary na Yugoslavia kusomea ukocha.

Hilo halipo tena. Soka ni biashara, ngumi ni biashara, kikapu hali kadhalika na hata riadha.

Michezo hiyo yote inaweza kuingiza mabilioni ya fedha iwapo viongozi wake watakuwa na mipango madhubuti ya maendeleo.

Sasa klabu zinatumia hadi Sh100 milioni kumnunua mchezaji kutoka nchi jirani ya Zambia tu. Sasa mchezaji analipwa mshahara hadi Sh5 milioni kwa mwezi. Sasa mwanariadha anayeshiriki Tokyo Marathon hakosi kurudi na kitita cha Sh10 milioni akifanya vizuri. Sasa Chama cha Riadha Tanzania (RT) hakiwezi kukosa udhamini wa Sh3 bilioni kwa mwaka kutoka makampuni ya vifaa vya michezo kama kitakuwa na mipango thabiti ya kuhakikisha timu ya taifa inashiriki vizuri Michezo ya Olimpiki, Afrika na mashindano ya dunia.

Iweje basi vyama hivi au wanamichezo hawa washindwe kulipia kodi ya vifaa ya Sh40 milioni? Ni Serikali gani itakubali kuondoa kodi katika mazingira kama hayo na kuacha viongozi wa michezo wakitumbua pesa ambazo zingechangia maendeleo ya Taifa?

Kwa hiyo, kuishi kwa dhana ya kizamani katika dunia ya sasa ndiko kunakotufanya tuendelea kutegemea huruma ya serikali katika kila kitu.

Lakini viongozi hawa hawa wanapokuwa kwenye kampeni ndio hutoa ahadi lukuki za kuinua uchumi wa vyama au klabu kwa kuweka mipango madhubuti ya maendeleo.

Sijui mipango hiyo huishia wapi na kugeuka kuwa kilio cha kuomba msaada kwa serikali.

Najua leo hii Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiitisha kikao cha viongozi wa vyama vya michezo, hakuna hata mmoja atakayekuwa ameandaa hoja za kuishawishi serikali kwamba iwapo itaondoa kodi kwenye vifaa vya michezo, katika muda wa miaka mitano au kumi ijayo michezo itakuwa inachangia kiasi gani katika Pato la Taifa, itakuwa imeajiri vijana wangapi, na itakuwa imesaidia kwa kiasi gani masuala ya kijamii.

Na kuondoa kodi katika vifaa vya michezo maana yake nini? Vifaa vya mafunzo? Vifaa vya mafunzo vitatenganishwaje na vifaa vya mashindano? Vifaa vya michezo kwa watoto? Na kwa nini iwe michezo na si nyanja nyingine?

Haya ndiyo mambo ambayo serikali inatakiwa iambiwe ili ifikirie cha kufanya katika kupunguza mzigo wa kodi kwa wanamichezo.

Kuiambia serikali kwamba vifaa vya michezo vikiondolewa kodi, nchi itapiga hatua mbele kimichezo, haitoshi kuishawishi kuondoa kodi kwa sababu ipo mifano ya sehemu nyingi ambazo michezo inafanya vizuri na kodi inalipwa.

Kwa hiyo suala la serikali kuchangia maendeleo ya michezo, halitakiwi liwe la kukurupuka. Viongozi wa michezo wanatakiwa kukaa pamoja na kutengeneza hoja zitakazoshawishi kuwa suala hilo likifanyiwa kazi mchango wa michezo unaweza kuwa mkubwa katika uchumi wa nchi na ustawi wa jamii.

Si blah blah kama anavyosema Darasa.