Mkutano utumike kujiweka sawa Jangwani

Muktasari:

  • Mkutano huo umepangwa kufanyika Oktoba 23, ikiwa ni wiki mbili tu zijazo ambapo moja ya ajenda inayotazamiwa kujadiliwa kwenye mkutano huo ni suala zima la mkataba huo wa Yanga na Yanga Yetu Limited.

UONGOZI wa klabu ya Yanga umeitisha Mkutano Maalum wa wanachama wake kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali, lakini kubwa likiwa ni suala zima la mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji wa klabu yao.

Yanga ipo kwenye mchakato wa kumkabidhi Mwenyekiti wao klabu hiyo kuiendesha kama mwekezaji mkodishiwa, ambapo tayari Mkataba baina ya Yanga na Kampuni ya Yanga Yetu Limited, umeshafanyika na kuibua sintofahamu baina ya wanachama wa klabu hiyo, viongozi wa Yanga na serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Mkutano huo umepangwa kufanyika Oktoba 23, ikiwa ni wiki mbili tu zijazo ambapo moja ya ajenda inayotazamiwa kujadiliwa kwenye mkutano huo ni suala zima la mkataba huo wa Yanga na Yanga Yetu Limited.

Yanga imeamua kuitisha mkutano huo kutokana na mkanganyiko uliojitokeza siku chache baada ya BMT kupitia Kaimu Katibu Mkuu wake, Mohammed Kiganja kutoa ufafanuzi wa kipi kinachopaswa kufanywa na klabu hiyo, licha ya kuwa imeshasainishiana mkataba na mwekezaji wao.

Kauli hiyo ya Kiganja imesababisha viongozi wa Yanga kumjibu, huku wanachama wa Yanga wakiwa wamegawanyika, wapo wanaounga mkono msimamo wa serikali na wengine kuona kama baraza hilo linawaingilia kwenye mambo yao.

Lakini kwa kuwa uongozi umeshakata mzizi wa fitina kuitisha mkutano huo ili kuweza kuweka mambo hadharani na pengine kurekebisha hali ya mambo yaliyopo klabuni kwao, Mwanaspoti linaamini mkutano huo utakuwa na tija kwa mustakabali wa klabu hiyo.

Hiyo ni fursa nzuri kwa wanayanga kujadiliana kwa hoja katika kuhakikisha kila kitu kinaenda vema katika mchakato wao wa kutaka kuifanya Yanga iendeshwe kisasa, ikizingatiwa kuwa, dunia ya sasa ndivyo inavyotaka klabu za soka ziwe.

Haitarajiwi mkutano huo uwe chanzo cha kuvuruga mambo ndani ya Yanga. Viongozi walioitisha lazima watoe ufafanuzi wa kutosha katika jambo lililopo mbele yao, ikiwemo kutoa nafasi kwa wanachama wao kuhoji na kuamua kile ambacho wanakiona ni sahihi.

Mkutano huo usitumike kama mahakama ya kuwahukumu wanachama ambao wana misimamo tofauti na viongozi. Tunalisema hili kwa kurejea mkutano wa dharura uliofanyika Agosti mwaka huu, ambapo kuna baadhi ya wanachama walifukuzwa uanachama wakiwamo Wajumbe wa kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.

Hatutaki kuingilia mamlaka ya klabu hiyo, lakini kama wadau wa soka tulikuwa na hamu kubwa ya kutaka kuona mkutano huo unakuwa na tija na kuweka mambo sawa ndani ya Yanga ili kile wanachotaka kukifanya kiwe na baraka za watu wote na kuiepushia klabu hiyo mgogoro usio na maana yoyote.

Katika taasisi yoyote tofauti na mawazo na misimamo lazima iwepo, lakini kila upande ni lazima usikilize na kuheshimu hoja za wenzao kama zina manufaa kwa mustakabali wa klabu yao.

Yanga ni klabu ya wanachama na kila mmoja ana haki ya kutaka kuona klabu yao inatengemaa mambo yake na kujiondoa mahali ilipo, ambapo kwa miaka zaidi ya 80 bado imekuwa tegemezi wakati ina utajiri wa kutosha wa kuweza kuifanya ijiendeshe kitajiri.

Ndio maana Mwanaspoti linasisitiza tena Mkutano ujao wa Yanga utumiwe vema kwa manufaa na maendeleo ya klabu hiyo na katu usitumike kuwa chanzo cha kuanzisha mgogoro utakaokuja kuitafuna Yanga, ikizingatiwa kuwa vita ya panzi siku zote huwa ni furaha ya Kunguru.

Kama wanachama wa Yanga na viongozi wao hawatakuwa makini katika kuutumia mkutano huo kuweka mambo yao sawa, wasije wakamtafuta mchawi mbele ya safari.

Pia ni msisitizo wetu kuwa, mkutano huo usitumike kama sehemu ya kuendeleza malumbano yao na BMT kwani kufanya hivyo hakuwezi kusaidia kuweka mambo yao sawa.

Inawezekana ni kweli BMT imewakwaza viongozi wa Yanga na baadhi ya wanachama wanaounga kilichofanyika mpaka sasa, lakini busara na hekima ni lazima itumike katika kuhakikisha kile wanachokikusudia kukifanya kulekea kwenye mfumo mpya.

Yanga ni taasisi kubwa yenye watu wa kada mbalimbali wakiwamo wasomi, hivyo ni wajibu wa kufanya mambo yao kwa akili ilimradi hawakiuki taratibu, katiba yao na hata sheria za nchi.

Kama wanayanga watafanya uzembe wowote kwenye mkutano huo, basi wakae wakijua hawakuwa na wa kumlaumu.