Mkamba anavyonishangaa habari ya Adebayor kuja Yanga

Tuesday February 7 2017

 

JUMANNE iliyopita niliandika mshangao wangu kwa Watanzania ambao walikuwa wanaamini kuwa Emmanuel Adebayor anaweza kuja kusajiliwa na Yanga.

Lakini msomaji wa Gazeti la Mwanaspoti ambaye pia ni mchambuzi wa soka kutoka Morogoro, Ibrahim Jaffar Mkamba, naye amenishangaa kwa nini nashangaa jambo hilo. Msome Mkamba alichoakiandika.

Kaka Frank, habari za kazi. Kila Jumanne huwa sikosi makala zako kwani huwa unachambua mambo ya soka kwa kina ukitumia fasihi kali, lakini ya lugha nyepesi. Toleo la Mwanaspoti la Jumanne  iliyopita (31/1-1/2/2017, namba 2223) uliandika makala iliyonisisimua sana kuhusu habari ya kuja kwa Emmanuel Adebayor Yanga ukieleza kwa umahiri mkubwa sababu za kiuchumi za kutotekelezeka kwa jambo hilo.

Frank uko Tanzania na Tanzania si nchi ya soka la ushindani wa kuwania mafanikio kimataifa. Tuna soka la kuzomeana na kukejeliana Simba na Yanga, tuna soka la wachezaji wa timu zisizo Simba au Yanga kucheza dhidi ya timu hizo kwa mapenzi au chuki kulingana na wachezaji wa timu hizo nyingine wanashabikia Simba au Yanga!

Utaona beki imara wa timu pinzani akifanya makosa ya kijinga anapocheza dhidi ya moja ya timu hizo kubwa, lakini akawa imara na makini akicheza na nyingine!

Hii unaweza ukaisema ni ya kimchezo, lakini kwa nini itokee hivyo kwa mechi zote dhidi ya timu hizo? Kwa nini makosa hayo yawe ya kunufaisha timu moja tu kila mechi? Hali ni hiyo hiyo kwa viungo na washambuliaji. Wachezaji wa ushabiki wa kitoto namna hiyo wana ndoto zipi? Kufika wapi kisoka? 

Hatuna nia ya wazi ya kucheza soka ya kulipwa nje. Si lazima kuchezea timu kubwa za Ulaya. Kwa mfano beki kisiki wa Cameroon mwenye ndevu za kidevuni alizozipaka rangi, Adolphe Teikeu, anachezea Sochaux ya League 2 ya Ufaransa huku mchezaji wao machachari aliyefunga bao la pili la ‘counter attack’ dhidi ya Ghana kwenye nusu fainali ya Afcon mwaka huu, Christian Bassogog, anachezea timu iitwayo AaB ya Denmark. Wachezaji wetu wengi wanaweza kuchezea timu za kawaida za Ulaya kama hizo, lakini hawana ndoto hiyo na hivyo hawajijengi kwenda huko. Kwa jumla hatuko kwenye soka ya ushindani wa kimataifa ila tuko kwa ushindani wetu hapa, ndani na nje ya uwanja; nje yenyewe ya uwanja ni nje ya viwanja vya umma huku timu zetu zikiwa hazina viwanja vyao vya hadhi isipokuwa Azam tu.

Hapa nalizungumzia soka la Tanzania lenye kanuni za kipekee duniani ya kuotea! Hapa, mara nyingi mchezaji akionekana ametangulia tu kuelekea lango la timu pinzani wadau wengi huamini ameotea bila kujali wakati mpira unapigwa kwake alikuwa wapi. Tutawalaumu waamuzi wasaidizi lakini wachezaji wa timu inayoshambulia hawaonyeshi kujua wamedhulumiwa, wachezaji wa timu inayoshambuliwa hawajui walimuweka mshambuliaji kwenye sehemu isiyo ya kuotea, watazamaji hawajui na hata baadhi ya watangazaji na waandishi hawajui!

Umeshangaa ya Adebayor na nimekushangaa, lakini ningekushangaa zaidi ungeshangaa sisi kukosa waamuzi kwenye mashindano makubwa ya bara hili ambapo hata Djibout, Seychelles na Mauritius huwa wanatoa waamuzi kwenye mashindano hayo.

Kaka Frank, kama kilele chetu cha soka si Yanga na Simba, kwa nini nchi ilikuwa baridi kabisa wakati ilipotangazwa tumeshinda rufani yetu dhidi ya Congo kwenye mashindano ya umri wa chini ya miaka 17?

Ona, habari iliyoifunika hiyo ni ya Yanga kuongeza pengo la alama kufikia nne dhidi ya Simba na wala si ya Tanzania kuingia fainali ya vijana Afrika! Hayo si yetu, yetu ni ya Simba na Yanga tu.

Kwa nini unashangaa habari ya Adebayor wakati hapa kwetu mashabiki wa timu inayoongoza ligi kwa tofauti ya alama mbili wanazomewa na wenzao walio nyuma kwa alama hizo kiasi cha wale wa timu inayoongoza ligi kukosa raha?

Hicho ndicho kilele cha burudani yetu ya soka. Unashangaa nini wakati dunia nyingine inawaona wachezaji kama Obrey Chirwa wa Yanga, Laudit Mavugo na Juuko Murshid wa Simba kuwa na viwango vya kucheza ligi kubwa kuliko hii sisi tukiwaona magalasa kwa kutojua kwetu soka? 

Katika mazingira hayo unashangaa nini kusemwa Adebayor anakuja kuchezea Yanga, wakati hatuna burudani za soka zaidi ya hizo za kuzomeana na kuambiana habari za kusisimua?

Shangaa hiyo kabla hujashangaa kubwa itakayoshushwa hivi karibuni ya kocha wa Leicester City, Claudio Ranieri, kuja kuifundisha Simba. Mpira umetushinda kimataifa, kwa nini tusiburudike na habari za kina Adebayor wa kimataifa? Hii ndiyo sababu nakushangaa Frank kushangaa habari ya Adebayor kuja kuchezea Yanga labda wewe si Mtanzania.