Miaka 50 ijayo huenda Ligi Kuu Bara itakuwa imekufa

Tuesday March 28 2017

 

By FRANK SANGA

NAANGALIA miaka 50 ijayo, huenda Ligi Kuu Bara itakuwa haipo. Si kwamba nipo ndotoni. Naangalia kwa jicho la kichokozi.

Jambo linalonitia shaka ni kuona kadiri ligi yetu inavyodorora ndivyo jinsi Ligi Kuu England inavyopanda na kuzidi kuwa maarufu.

Vijana wanaozaliwa sasa, hawaijui Simba wala Yanga. Wanaijua Chelsea, Manchester United, Arsenal, Liverpool na nyinginezo za Ulaya.

Ukiwauliza watoto wengi wa miaka mitano, watakwambia wanashabikia timu hizo za Ulaya na kwamba kwa Tanzania hawana timu yoyote. Inaumiza kusikia majibu hayo, kwa sababu hata mashabiki ambao wanakwenda uwanjani sasa, ni kwa sababu ya timu mbili tu; Simba na Yanga, vinginevyo wasingekuwa wanakwenda viwanjani.

Lakini kadiri miaka inavyokwenda inaelekea hata Simba na Yanga zinapoteza mvuto au zimeshindwa kujitengenezea jina mbele ya kizazi kipya. Sijakosa mechi ya Simba na Yanga, ni lini mara ya mwisho Uwanja wa Taifa umejaa katika mechi ya watani wa jadi?

Bila mechi za Ligi Kuu England, kila kitu kinakuwa kimepoa. Ukitaka kujua hilo, angalia jinsi wikiendi iliyopita ilivyokuwa imepoa.

Ilikuwa wikiendi nzuri kwa upande fulani. Kwa sababu Taifa Stars ilishinda katika pambano lake la kimataifa la kirafiki dhidi ya Botswana.

Mbwana Samatta alifunga mabao yote mawili katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na inaonyesha jinsi tunahitaji vijana wengi kwenda kucheza soka Ulaya.

Lakini, ilikuwa wikiendi iliyopoa kwa sababu hakukuwa na Ligi Kuu England, ambayo huwaweka watu katika mshikemshike Jumamosi na Jumapili.

Inawezekana Ligi Kuu England ikawa inaangalia kuliko kitu kingine chochote duniani. Inaweza kuzidiwa na fainali za Kombe la Dunia tu.

Je, kama watu wamekuwa wakiisubiri kwa hamu kubwa Ligi ya England, hii ina maana kuwa ligi zetu za ndani zipo shakani na zinaweza kupotea wakati wowote.

Ukienda Uganda, mashabiki hawaendi uwanjani. Wanakwenda kwenye mechi ya watani wa wajadi tu; Express dhidi ya SC Villa.

Kenya nako ligi yao imepoteza mvuto, mashabiki wanakwenda uwanjani inapokuwa mechi ya watani; Gor Mahia na AFC Leopards tu. Lakini katika nchi hizo, kuna mashabiki wengi wa Ligi Kuu England pengine kuliko hata Tanzania. Kenya na Uganda mashabiki wa jinsia zote wamekuwa wakijazana sehemu za starehe kwa ajili ya kufuatilia ligi hiyo yenye timu 20.

Tanzania si kisiwa, ni sehemu ya dunia. Ni nchi ambayo tumekuwa tunapokea mabadiliko ya teknolojia kwa kasi sana. Kwa hiyo haitakuwa ajabu kuona mashabiki wakiacha kwenda kwenye viwanja vya soka miaka michache ijayo. Kuna dalili zote za jambo hilo, kwa sababu Uwanja wa Taifa umekuwa haujazi tena mashabiki. Hata mechi ya Simba na Yanga imekuwa haijazi tena uwanja.

Mashabiki 60,000 si wengi, lakini Uwanja wa Taifa umekuwa ukifikisha mashabiki 45,000 tu katika mechi kubwa ya watani Simba na Yanga. Katika mechi nyingine za kawaida imekuwa ni aibu tupu na kuna dalili zote kuwa miaka miwili ijayo tusipokuwa makini viwanja hivyo vitakuwa vitupu kabisa.

Timu zitakuwa zinakwenda uwanjani kucheza kwa ajili ya kujihakikisha kubaki katika Ligi Kuu Bara, au kupata nafasi ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa.

Tatizo jingine viwanja vyetu havina starehe nyingine zaidi ya soka ambalo limepoteza mvuto na sasa watu wamehamia Ligi Kuu England.

Viwanja havina baa, migahawa, michezo ya watoto wala maduka makubwa.

Wakati viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiwa katika kampeni kubwa ya kuhakikisha wanarejea madarakani, ni vyema wakaanza kuchukua hatua kujua sababu zinazowakimbiza watu viwanjani.

Ni aibu kubwa viongozi hawa kujikuta wakisimamia ligi ambayo haina mashabiki, na kama haina mashabiki haitakuwa na wadhamini na haitakuwa ikionyeshwa na televisheni.

Kazi kwenu.