MTAA WA KATI : Huu ndiyo ubora wa Jose Mourinho

Muktasari:

  • Mourinho anawasukuma wachezaji wake na kuwazaja maneno ya hamasa muda wote kuwa wao ni machampioni, inalipa na anakusanya mataji ya kutosha. Wenger anaendelea na falsafa zake za kufundisha mpira akiamini mtu kama Olivier Giroud atakuwa kama Cristiano Ronaldo. Huo ndio ubora wake Wenger. Ana maksi zake hapo.

JOSE Mourinho ni tofauti na Arsene Wenger. Wenger anafundisha kucheza mpira. Mourinho anataka wachapakazi..

Mourinho anawasukuma wachezaji wake na kuwazaja maneno ya hamasa muda wote kuwa wao ni machampioni, inalipa na anakusanya mataji ya kutosha. Wenger anaendelea na falsafa zake za kufundisha mpira akiamini mtu kama Olivier Giroud atakuwa kama Cristiano Ronaldo. Huo ndio ubora wake Wenger. Ana maksi zake hapo.

Kwa upande wa Mourinho pamoja na kuhitaji wachezaji ambao tayari wametengenezwa kwa viwango na makocha wengine, lakini ana ubora wake. Ubora wa Mourinho ambao unamfanya awe na maksi za kutosha ni namna anavyowatumia wachezaji hao waliokwisha andaliwa.

Unamjua Marouane Fellaini? Umemwona anavyocheza kwa sasa Man United. Umeona kiwango chake? Mechi mbili za ligi, kiwango supa kabisa. Tena katika eneo lilelile ambalo alionekana hawezi kulimudu vyema.

Fellaini aliyekuwa akilalamikiwa kucheza sana viwiko. Halikuonekana hilo. Anachokifanya ni kutimiza wajibu wake kwenye sehemu ya kiungo, tena akicheza kwa nidhamu kubwa bila ya vurugu yoyote. Hakuwa kipenzi cha mashabiki, lakini sasa wameanza kumkubali taratibu. Kwa kiwango chake alichocheza msimu uliopita, Fellaini alikuwa mchezaji wa kwanza kutajwa kwamba asingeweza kuendelea kubaki OT chini ya Mourinho. Lakini, sasa Mbelgiji huyo amethibitisha kinyume na sasa ni mtu mwenye uhakika wa kupata namba muda wote kama tu Man United itahitaji kuendelea kuona ubora wa Pogba ndani ya uwanja.

Mourinho anafahamu wazi kupata huduma nzuri ya Pogba ndani ya uwanja, atahitaji kuwa na Fellaini kwenye kikosi. Kazi ya Fellaini ambayo amepangiwa na Mourinho ni kufanya shughuli za kukaba na kuvuruga mbinu za wapinzani huku jambo hilo likitoa nafasi kwa kiungo Pogba kucheza kwa uhuru goli hadi goli. Mourinho amefahamu wazi anahitaji watu kama Fellaini, ambao watahitaji kuthibitisha kwa mashabiki kwamba anastahili kuvaa jezi za timu yao ili yeye apate mafanikio. Fellaini anataka kuwathibitishia mashabiki wa Man United kwamba anastahili kuwa hapo. Hapa ndipo ulipo ubora wa Mourinho, hawezi kumwaacha mchezaji wa aina hiyo. Amemrudisha Pogba OT akimtaka awathibitishie mashabiki wa timu hiyo kwamba walifanya makosa kumwaacha aondoke hapo awali. Amemleta Zlatan kwenye timu yake kwa sababu fowadi huyo atataka kuonyesha kwamba ni straika asiyekuwa na mipaka kwenye kufunga mabao, anafanya hivyo kwenye ligi yoyote ile hapa duniani. Bailly alimwona kuwa ni beki mchanga na mwenye uchu wa mafanikio. Kama huna sababu maalumu huwezi kucheza kwenye kikosi cha Mourinho. Juan Mata wa sasa si yule wa miaka michache iliyopita. Unaona anavyoshughulika na shughuli za kukaba uwanjani kwa sasa. Anafanya hivyo kunusuru ajira yake kwa sababu bosi ndicho kitu anachokitaka. Ilikuwa rahisi sana kumwondoa Schweinsteiger kwenye mipango yake. Anafahamu wazi Mjerumani huyo hana kiu tena ya mafanikio. Kipindi chake cha mapambano kimekwisha. Mourinho hafundishi mpira, anamfundisha mchezaji mbinu za kuutumia ubora wake. Huo ndio ubora wa Mourinho.