JICHO LA MWEWE: Kuna sababu moja tu ya kupenda soka la Tanzania

Muktasari:

  • Unajiuliza kimeshindikana nini kuifanya sehemu ya kuchezea uwanjani iwe na nyasi safi na zenye viwango

MAISHA magumu, hasa haya ya Rais JPM ambayo hatukuyazoea. Ni maisha halisi sana. Ujanja ujanja umetoweka na pesa ya haraka haraka imetoweka. Baada ya shida ya mchana kutwa, jioni inawadia na unahitaji kupumzika.

Na baada ya shida za wiki nzima, wikiendi inawadia na unahitaji kupumzika. Kwa wapenzi wa soka ni rahisi kuchukua rimoti yako na kuweka Ligi Kuu ya England. Ni rahisi sana na kuna sababu 100 za kupenda Ligi Kuu ya England, halafu kuna sababu moja tu ya kupenda Ligi Kuu ya Tanzania.

Kwa mfano, kwanini upende soka la Tanzania hasa ligi yake wakati ukiwa getini tu kuingia uwanjani unasikia watu wanazungumzia rushwa ya mechi hiyo bila ya hofu. Siku hizi rushwa ipo hadharani sana tofauti na enzi za kina Hamis Gaga.

Unatazama mabao mazuri Uwanja wa Taifa au kwingineko, unajiridhisha kwamba umetazama soka. Mwisho wa siku unaambiwa kumbe mwamuzi alichukua pesa, kipa alichukua pesa, mabeki wake walichukua pesa. Hakuna kificho sana na wakati mwingine ushahidi wake upo hadharani.

Kocha Patrick Liewing alikuwa pale Stand United. Amesema wazi kwamba kuna wachezaji wake wamechukua pesa kutoka kwa timu pinzani. Nani amejali? Aliwataja wachezaji hadi kwa majina. Umesikia wameitwa TFF? Umesikia wameitwa Takukuru?

Sijui kwa nini neno rushwa au hujuma limeimarika sana na labda mambo haya hayakuwepo zamani kwa sababu wachezaji walikuwa mahiri sana na timu zilikuwa zinajiamini kushinda mechi kwa uwezo. Labda wachezaji wetu wa kizazi hiki ni wa kawaida sana kiasi kwamba, wanalazimika kusaidiwa na pesa kushinda mechi.

Achana na rushwa, unaposema gazeti unaambiwa wachezaji wa Simba hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu. Unajiuliza, kama Simba haijalipa wachezaji wake mishahara kwa miezi mitatu itakuwaje kwa Mbao FC?

Kama timu ambayo inaongoza kwa mashabiki nchini pamoja na mtani wake inashindwa kulipa mishahara, nani mwingine ataweza? Ni kama vile Manchester United ishindwe kulipa mishahara, Hull City itawezaje? Tunafanya masikhara na mpira. Inapofika hapo unahamisha rimoti yako kuangalia mechi ya Tottenham na Arsenal pale London.

Achana na hilo, unajaribu kutazama mechi kati ya Majimaji ya Songea na Toto Africans pale Songea. Unashindwa kuelewa unatazama mpira au ng’ombe wanacheza katika zizi? Uwanja haueleweki. Uwanja una vilima na mabonde kibao.

Mchezaji anatumia akili mbili kabla ya kucheza mpira. Kwanza analazimika kupambana na uwanja, kisha anapambana na mpira. Huu ni uwanja wa Ligi Kuu au zizi la ng’ombe? Majukwaani kuna mashabiki lukuki. Unajiuliza kimeshindikana nini kuifanya sehemu ya kuchezea iwe na nyasi safi na zenye viwango.

Kinachoshindikana hapo ni kuusawazisha uwanja, kupanda nyasi safi, kisha kumwagilia. Unajiuliza, hata hili linahitaji hisani ya watu wa Marekani? Kufikia hapo unahamisha ulichokuwa unatazama na unaweza pambano kati ya Chelsea na Everton. Unakutana na soka safi ambalo unaamini kuwa atakayefungwa anafungwa kwa sababu amezidiwa uwezo na sio kwa sababu ya rushwa au uwanja mbovu ama hujuma.

Vipi kuhusu ratiba ya ligi? Hapa napo kuna vichekesho sana. Ratiba inatoka mapema, lakini unajua kuwa haitakwenda kama ilivyo. Rafiki yangu mmoja, Jurgen Malima alikuwa Mbeya wikiendi hii akila kuku kwa mrija bila ya kupenda. Sikiliza kisa chake.

Katika ratiba ya awali mechi ya Simba na Prisons ilipaswa kucheza wikiendi hii ya jana. Baadaye ikarudishwa nyuma mpaka ile Jumatano kwa ajili ya kupisha mechi ya Stars ya leo. Malima alishakata tiketi mapema kwa ajili ya mechi ya wikiendi hii. Amelazimika tu kwenda Mbeya kuendelea na starehe zake kwa sababu ya mabadiliko ya ratiba.

TFF haikujua kama wikiendi hii kuna ratiba ya mechi za kimataifa tena ambazo zipo chini ya Fifa? Unapofika hapo ndipo unapohamisha na kuangalia mechi za maana za wenzetu. Ratiba ya Ligi Kuu ya England inapangwa Agosti inamalizika Mei bila ya kubadilisha hata mechi moja labda itokee janga na si vinginevyo.

Kufikia hapo unabakiwa na sababu moja tu ya kulipenda soka la Tanzania. Tunalipenda kwa sababu ni soka letu la nyumbani. Hatuna sababu ya msingi sana ya kulipenda ndani na nje ya uwanja. Ni vile tu inaitwa Ligi Kuu ya Tanzania na watu wengine wanalazimika kwenda uwanjani kwa sababu hawana sehemu ya kwenda, na wengine ni kwa sababu wamerithi mapenzi ya timu. Kama tunaamua kutafuta sababu za kupenda hatuwezi kupata hata moja ya msingi sana zaidi ya Utanzania wetu. Na kama tunaamua kutafuta sababu za kupenda La Liga au Ligi Kuu ya England basi tunaweza kupata mia za msingi zaidi tena za wazi kabisa sio za kuunga unga.

Kitu cha msingi zaidi kwa sasa ni kuhakikisha tunapata First Eleven ya timu ya taifa inayotoka Ulaya. Watafikaje? Sijui. Lakini kwa kufuatilia soka la ndani linavyochezwa, hasa Ligi Kuu, unaweza kutapika sebuleni muda wowote ule ama ukaamua kuvunja luninga kwa hasira.