Kombe la Mapinduzi liendeshwe kwa kanuni

Friday January 6 2017

 

By MWANASPOTI

MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi 2017 inayoendelea kushika kasi visiwani Zanzibar, imekuwa na msisimko mkubwa katika msimu wake wa 11.

Ushindani uliopo kwa klabu shiriki umeifanya izidi kuwa kivutio katika ukanda wa Afrika Mashariki, hasa baada ya kupoteza mvuto kwa michuano mingine inayoendeshwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), ikiwemo ile ya Kagame Cup.

Uwepo wa klabu kubwa na maarufu za ukanda huo kama Simba, Yanga na Azam na klabu waalikwa kutoka nje ya nchi, imefanya kila mdau wa soka kuifuatilia kwa kina kufahamu kinachoendelea katika michuano hiyo ambayo inarushwa live na luninga ya Azam Tv.

Kwa wanaoifuatilia michuano hiyo wanaweza kukubaliana na Mwanaspoti kuwa msimu huu ushindani umekuwa mkubwa, kiasi cha kushuhudia hata klabu wenyeji za Zanzibar zikikataa kuwa jamvi la wageni.

Pamoja na ushindani na mvuto mkubwa uliopo kwenye michuano hiyo ambayo iliasisiwa mwaka 2007 katika mfumo unaotumika kwa sasa, kuna mambo ambayo Kamati inayoratibu inapaswa kurekebisha ili mambo yazidi kusisimua.

Kubwa ni kuhakikisha michuano hiyo inapata wadhamini wa kutosha ambao, watasaidia kuifanya iwe na zawadi nono zitakazochochea ushindani na kusaidia kwa namna moja ama nyingine kukuza soka la ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Zawadi za michuano hiyo kwa hakika ni ndogo kulingana na hadhi ya michuano hiyo inayokumbushia historia ya Mapinduzi yaliyofanyika visiwani huo yaliyowakomboa Wazanzibar mnamo Januari 12, 1964.

Haiwezekani michuano inayoelekea kuwa ya kimataifa kuendelea kutoa zawadi ambazo zinashindwa hata na michuano ya mchangani ya Ndondo Super Cup iliyomalizika katikati ya mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Mbali na hilo la zawadi ambalo linaweza kuchagiza hata kuongezwa kwa idadi ya timu shiriki hasa kutoka nje ili kuongeza utamu zaidi, lakini Kamati ya michuano hiyo inapaswa kuweka kanuni zitakazoipa heshima michuano yao. Heshima ndio msingi wa maendeleo.

Mwanaspoti inalisema hili kutokana na kitendo kilichojiri mapema wiki hii katika michuano hiyo kwa mchezaji Abdi Kassim ‘Babi’ kuruhusiwa kuzichezea timu mbili tofauti katika michuno ya msimu mmoja.

Babi alikuwa akiicheza Taifa ya Jang’ombe ‘Wakombozi wa Ng’ambo’ na alikuwapo katika kikosi kilichovaana na Jang’ombe Boys siku ya ufunguzi wa michuano hiyo Ijumaa iliyopita.

Katika mchezo huo Taifa iliitambia Boys kwa bao 1-0, lakini siku chache baadaye Babi aliibukia klabu ya Boys saa chache baada ya kuhama Taifa klabu zilizo na upinzani wa jadi visiwani humo.

Yaani mtu amesajiliwa asubuhi, kisha jioni anacheza michuano ambayo ilishaanza na kushika kasi, ni kituko cha mwaka, lakini hii ni kwa sababu michuano hiyo haina kanuni za usajili zinazoiongoza na kuifanya iheshimiwe.

Hata kwenye Ndondo Cup na michuano mingine ya mchangani ina kanuni ambazo zinaifanya michuano hiyo ieleweke, ingawa Mwanaspoti haipendi kutaka kuifundisha kazi Kamati ya mashindano hayo.

Inawezekana Babi amehama Taifa na kutua Boys kwa vile dirisha dogo la usajili la Ligi za visiwani humo limeshafunguliwa tangu Desemba 15, mwaka jana, na likitarajiwa kufungwa Januari 15, mwaka huu, lakini hatudhani kama alistahili kuanza kuichezea timu yake mpya katika michuano ambayo alishacheza na timu nyingine.

Ndio maana tunaikumbusha Kamati ya Mashindano hayo, ili kuepuka kujitia aibu na kuishushia heshima michuano hiyo, lazima iweke kanuni za usajili na maeneo mengine ili angalau kupandisha hadhi yake mbele ya timu ngeni ambazo zinatoka nje ya nchi.

Kanuni ndio zitazifanya timu shiriki kufuata utaratibu na hivyo, kuepusha malalamiko yasiyo na tija.