Kitumbo Raiola anavyotamba Lowry Hotel Manchester kwa noti za usajili

Muktasari:

Jose Mourinho huwa analala Lowry mpaka sasa kwa sababu hajatafuta nyumba Manchester. Wachezaji wapya wa Manchester United na Manchester City huwa wanakaa Lowry kabla ya kutafuta nyumba za kuhamia.

THE Lowry Hotel. Hoteli moja hivi ya kifahari katika Jiji la Manchester. Kuna chumba kimoja kinagharimu Sh4 milioni kwa usiku mmoja. Ndipo Manchester United wanapokusanyika kupanda basi kwenda uwanjani. Wakati mwingine hukusanyika wanaposafiri kwenda miji mingine.

Jose Mourinho huwa analala Lowry mpaka sasa kwa sababu hajatafuta nyumba Manchester. Wachezaji wapya wa Manchester United na Manchester City huwa wanakaa Lowry kabla ya kutafuta nyumba za kuhamia.

Kevin de Bruyne alilala hapo. Henrikh Mkhitaryan alilala hapo. Nolito alilala hapo. Ni bonge la hoteli. Kwa sababu mastaa wa United na City wanalala hapo, majuzi wamiliki wa hoteli walitengeneza upya gym na chumba cha kupashia misuli joto kwa mvuke (sauna) kwa Pauni 4 milioni. Unahitaji nini tena ukiwa Lowry.

Hizi wiki mbili kila nikiifuatilia Hoteli ya Lowry nagundua imepata mteja mpya. Kibonge cha mtu hivi. Hahitaji gym yao wala sauna. Kajinenepea tu. Anakula kila saa. Anaitwa Mino Raiola. Wakala wa Zlatan Ibrahimovic. Pia ndiye wakala wa Romelu Lukaku. Ndiye wakala wa Mario Balotelli. Ndiye wakala wa Paul Pogba na mwaka jana alikamilisha uhamisho uliovunja rekodi ya dunia na yeye mwenyewe akatia mfukoni Pauni 20 milioni. Peke yake!

Mambo yameiva kwa Raiola mpenda pesa. Amejivuta England kwa sababu wateja wake wawili wamempa cha kuongea. Wa kwanza ni Zlatan. United ilimchukua Zlatan kwa mkataba wa mwaka mmoja tu akitokea PSG.

Sasa mkataba wake umebakiza miezi miwili tu. Hivi umewahi kujiuliza, United bila ya Zlatan ingekuwa ya ngapi katika msimamo wa Ligi Kuu England? Umewahi kujiuliza, United bila ya Zlatan ingetwaa vipi Kombe la Ligi? Umewahi kujiuliza kama United ingeendelea kuwepo katika michuano ya Kombe la Europa?

Ana mabao 26 safi mpaka sasa pale Old Trafford. Vijana wadogo kina Marcus Rashord na mkongwe wao, Wayne Rooney wanaonekana kutepeta mbele ya Zlatan. Kwa nini Raiola asifunge safari ya mapema kuja Lowry Hoteli kuanza kufanya biashara?

Ametua Lowry kifua mbele. Amekuja na kelele kweli. Huyu ni mmoja kati ya wateja wake wanaompa jeuri. Kwa sasa anaitaka kuigeuza United mateka. Anajua kwamba United inamhitaji Zlatan kuliko Zlatan anavyoihitaji United. Tayari Raiola ameshaanza kelele zake. Anadai kuwa Zlatan ana ofa ya mshahara mkubwa kutoka Marekani na China. Lengo hapa ni kuhakikisha United inapanda dau kweli kweli kumbakisha Zlatan Old Trafford msimu ujao.

Kadiri United itakavyolipa pesa nene ndivyo na yeye asilimia zake zitakuwa nene zaidi. Raiola anacheka tu huku anakuna kitambi chake. Ndani ya moyo wake, Zlatan atakuwa anafurahia kucheza soka la kiushindani Ulaya. Itakuwa anataka kubakia Old Trafford.

Hata hivyo, Raiola hawezi kukiri hili mapema mpaka kwanza awahenyeshe United.

Mteja mwingine ambaye amempa jeuri Raiola kwa sasa ni Lukaku. Huyu naye kwa msimu wa pili anampa jeuri. Tafuta msimamo wa wafungaji katika Ligi Kuu England, Lukaku ndiye anayeongoza. Ana mabao yake 21.

Kitu cha kwanza ambacho amefanya Raiola kwa sasa ni kutangaza kwamba Lukaku hatasaini mkataba mpya Goodson Park. Ni lazima Lukaku ataondoka mwishoni mwa msimu huu. Raiola yupo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba klabu kubwa zinampigania Lukaku.

Ni wazi kwamba klabu kama Manchester United, Chelsea, PSG zitapigana kuisaka saini ya Lukaku. Anachotaka Raiola ni pesa ndefu tu katika dili hili. Mate yanamtoka na tayari ametua kuangalia ofa ambazo zipo mezani kwa Lukaku. Zitakuwa nyingi.

Awali Lukaku alikuwa bado hajakomaa wakati ametua Chelsea akitokea Anderlecht akiwa na umri wa miaka wa 18. Baadaye akamhamisha kwenda Everton ambapo kwa sasa amekomaa. Sasa biashara ipo mezani.

Raiola anachekea tumboni kwa sababu ana biashara mbili zipo wazi mezani. Anaweza kuwa na wateja wengine lakini msimu huu biashara ambazo zipo wazi ni hii ya Zlatan na Lukaku. Kule Ufaransa kwa Balotelli ni kwamba inawezekana kweli anafanya vizuri lakini biashara bado haijakaa sawa. Labda msimu ujao.

Hapa kwa Pogba biashara bado haiwezekani. Kachukua pesa mwaka jana tu na Pogba ana mkataba wa miaka sita. Labda baada ya miaka miwili Raiola anaweza kufanya utundu fulani mwingine lakini kwa sasa biashara aliyoifanya kwa Pogba haiwezi kujirudia karibuni. Kwa sasa yupo Lowry kwa ajili ya biashara hizi mbili nzuri. Haya ndiyo maisha ya mawakala.

Bahati nzuri katika miezi ya karibuni Raiola amekuwa staa wa mchezo. Amewanyamazisha kabisa wakongwe wengine wa biashara hii kina Jorge Mendes na Pini Zahavi. Anatamba yeye tu sokoni kwa sasa. Wateja wake wanampa kiburi kwa kiasi kikubwa na sishangai kumwona akirandaranda katika kumbi za hoteli za Lowry.