HISIA ZANGU: Cannavaro, anahitaji maamuzi magumu, lakini hatayafanya

MECHi ya Simba na Yanga inapochezwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ yupo benchi, hakuna mtu anayeshangaa. Pambano linamalizika, hakuna anayeshangaa. Na mwisho wa yote mashabiki wanaondoka wakiamini hakuna ambacho labda Cannavaro angebadili katika mchezo. Yaani kila kitu ni poa tu.

Ukiona hivyo ujue kuna kitu. Ndiyo, kuna kitu hapa na imetokea wiki mbili zilizopita katika pambano la watani wa jadi. Cannavaro amekaa benchi akiwa chaguo la nne katika timu nyuma ya Vincent Bossou, Kelvin Yondani na staa mpya kikosini, Andrew Vincent ‘Dante’.

Miezi 24 iliyopita Nadir alikuwa lulu kweli kweli na ndiye alikuwa chaguo la kwanza. Sasa hivi sio lulu tena. Ni dhahiri kwamba nyakati zinampita Cannavaro, ambaye alikuwa mmoja kati ya walinzi wazuri waliotoa kila walichonacho katika jezi za Yanga na timu ya taifa.

Nadhani hata mwenyewe hawezi kubisha sana katika hilo na hautakutana na mchezaji mwenye nidhamu, akili, mtu mzuri, mpenda watu kama Nadir. Na nadhani ndio maana hawezi kubisha kwamba, nyakati zimemtupa mkono na anatakiwa kufanya kitu fulani.

Hata hivyo, wachezaji wetu wanakubali kilaini zaidi kwamba wamezeeka. Kwa mfano, ni wazi kwamba itakuwa ngumu kwa Cannavaro kuirudisha namba yake katika kikosi cha kwanza, nikichunguza jinsi mlinzi wao mpya, ‘Dante’ anavyocheza.

Pamoja na hilo, Cannavaro hajaisha sana kiasi cha kushindwa kucheza timu nyingi za Ligi Kuu nchini. Anaweza kuingia katika vikosi vingi vya kwanza vya klabu mbalimbali za Ligi Kuu achilia mbali zile kubwa ambazo katika nafasi hizo zina wachezaji imara zaidi wa kigeni.

Unaweza kumuona Cannavaro mjinga kwa kuendelea kusugua benchi wakati angeweza kucheza katika klabu mbalimbali za Ligi Kuu. Cannavaro sio mjinga. Kuna tofauti kubwa sana ya kiuchumi kati ya timu kubwa na ndogo.

Mshahara anaopewa Cannavaro Yanga ni afadhali kuendelea kukalia benchi katika timu hiyo kuliko kwenda kucheza Kagera Sugar au Mbeya City. Pengo hili la kiuchumi linaendelea kuimarika kila kukicha na hatuoni tatizo.

Kwa Ligi Kuu ya England, mchezaji aliyeisha Manchester United huku mshahara wake ukiwa pauni 150,000 kwa wiki kama Wayne Rooney, anaweza kurudi Everton na kupokea kiasi cha pauni 80,000 kwa wiki. Everton nayo ipo vizuri kiuchumi hata kama sio kwa kiasi cha kuilinganisha na Manchester United.

Tatizo kwa Cannavaro ni kwamba kama mshahara wake Yanga ni Sh. 2 milioni basi akienda Kagera Sugar atalipwa Sh. 500,000 kwa mwezi. Pengine huo ndio mshahara mkubwa klabuni hapo.  Hapa ndipo wachezaji wengi wa Simba, Yanga na Azam wanapoamua kusota benchi mpaka mikataba yao inapokwisha ili kulinda kipato chao.

Mkumbuke Nsajigwa Shadrack. Alipoondoka Yanga akaenda kujaribu Vietnam kidogo. Iliposhindikana akarudi akastaafu. Nadhani wachezaji wanaingiwa na uvivu wa kucheza katika timu za mishahara midogo, hasa kama walifikia katika viwango vya juu vya mishahara katika mikataba yao.

Kosa lingine ambalo wachezaji wetu wengi wamekuwa wakilifanya, pamoja na watu wa benchi la ufundi ni kutobadilisha majukumu ya wachezaji uwanjani pindi mambo yanapoanza kukataa.

Kwa mfano, nililaumu sana kuona Nsajigwa amekubali ameisha bila ya kuhama katika nafasi yake na kujaribu kucheza nafasi nyingine ili kuendelea kuwepo uwanjani.

Unapokuwa mlinzi wa kulia unakumbana na mawinga wenye kasi, lakini kama umri unakutupa mkono basi unaweza kusogea kucheza kama winga au ukaingia katikati kutumia uzoefu zaidi bila ya kasi. Wachezaji wetu wanacheza katika nafasi moja na wanastaafu katika nafasi hiyo hiyo, hawawezi kubadilika.

Ryan Giggs kasi yake ilipopungua alihamishiwa kucheza kama kiungo mshambuliaji na hiyo iliwahi pia kutokea nchini kwa mshambuliaji nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella. Alipoona hawezi tena purukushani za eneo la ushambuliaji pale katikati akajitoa na kucheza pembeni, huku akipiga zaidi mipira mirefu. Wataalamu wakampachika jina la DHL.

Cannavaro kwa sasa anaweza kujipima na kuanza kucheza kama kiungo mkabaji kama anataka kuendelea kuutumia mshahara wake mkubwa pale Yanga na kama hataki kwenda kucheza kwa mshahara mdogo. Ni kitu cha kawaida sana katika soka.

Mpaka sasa moja kati ya mijadala mikubwa inayoendelea katika soka la England ni sehemu mwafaka ambayo Rooney anapaswa kucheza kwa sasa katika klabu yake ya Manchester United au timu ya taifa ya England. Kasi yake imepungua na Waingereza wanajaribu kujua atacheza wapi ili aendelee kuwepo na kutengeneza rekodi zake mpya. Cannavaro naye anahitaji kufanya maamuzi magumu.