Klabu ziache kusajili kwa sababu ya kusaka sifa

Muktasari:

  • Simba imemleta kipa wa kimataifa kutoka Ghana, Daniel Agyei, wakati watani zao Yanga na Azam nao wakiwa wamevuta vifaa vya maana, ilihali klabu nyingine zikiendelea kujitutuma kwa kunyakua nyota waliopo nchini.

LIGI Kuu ya Vodacom kwa sasa ipo mapumzikoni, lakini pilikapilika iliyopo kwa sasa ni kwenye dirisha dogo la usajili.

Klabu 16 zinazoshiriki ligi hiyo zinachamgamkia zoezi hilo, nyingine zikisajili wachezaji na nyingine zikifanya mabadiliko ya mabenchi yao yao ya ufundi, ilimradi mapumziko ya ligi hiyo yasiende bure.

Simba, Yanga na Azam kama kawaida yao zinaendelea kuwa vinara wa kwenye zoezi hilo la usajili, likinyakua nyota wapya wa kitaifa na kimataifa, katika hali ya kuimarisha vikosi vyao.

Simba imemleta kipa wa kimataifa kutoka Ghana, Daniel Agyei, wakati watani zao Yanga na Azam nao wakiwa wamevuta vifaa vya maana, ilihali klabu nyingine zikiendelea kujitutuma kwa kunyakua nyota waliopo nchini.

Kwa namna usajili unaoendelea, mpaka dirisha hilo litakapofungwa Desemba 15 ni wazi mambo yatakuwa yameiva na timu zitaingia kwenye duru lijalo zikiwa kamili na kuongeza ushindani na mvuto wa ligi hiyo.

Hata hivyo wakati klabu zikiendelea kupigana vikumbo kwa ajili ya usajili wa wachezaji, Mwanaspoti lilikuwa linawakumbusha viongozi na mabenchi yao ya ufundi kufanya usajili wao kwa kuzingatia mahitaji ya timu zao. Viongozi ambao mara nyingi ndio wamekuwa wasimamiaji wakuu wa usajili wa klabu zao, wasifanye mambo kwa mihemko, kusaka sifa kwa wanachama na mashabiki wao ama kuonyesha kuwa hata wao wana uwezo kifedha. Sajili zote zifanywe kwa matakwa ya makocha wao kwa kuzingatia mahitaji ya timu husika. Katika kufuatilia zoezi linaloendelea kwa sasa, kuna baadhi ya klabu ni kama zinafanya usajili kwa kukurupuka ama kutaka nazo zionekane zimefanya usajili. Hatupendi kuziingilia klabu katika maamuzi yao, fedha ni zao, wanaowasajili ni kwa manufaa yao na timu zao, lakini kama wadau wa michezo tunawajibu wa kuzikumbusha kuwa usajili wa dirisha dogo ni wa marekebisho zaidi.

Klabu zinapaswa kusajili ama kuongeza wachezaji katika maeneo ambayo yameonekana yana mapungufu na sio kusajili ilimradi kwani klabu zinaweza kujiharibia kama watavivuruga vikosi vyao kipindi hiki kifupi. Kuna baadhi ya klabu ambazo zina matatizo katika nafasi za kiungo ama ushambuliaji, badala ya kusajili wachezaji wa maeneo hayo wanakimbilia kunasa mabeki ama makipa, hayo ni matumizi mabaya ya dirisha dogo. Klabu yenye tatizo la kipa ama beki, isajili wachezaji wa nafasi hizo na kama idara zao za ushambuliaji na kiungo zina walakini, huko ndiko kunakofaa kuimarishwa.