Yanga haijachelewa, haina haja ya kugombana na BMT

Muktasari:

  • Bahati nzuri mkataba huo umesainiwa, lakini siku chache baadaye serikali kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ilitoa msimamo wao juu ya jambo hilo na kutoa mapendekezo yake ili mambo yaende sawa Jangwani.

KATIKATI ya wiki iliyopita, Klabu ya Yanga ilitangaza hadharani kuingia mkataba na Kampuni ya Yanga Yetu Limited kwa ajili ya ukodishwaji wa klabu yao kwa miaka 10.

Suala hilo lilikuwa likifahamika kwa wanayanga tangu ulipofanyika Mkutano wa Dhararu miezi miwili iliyopita, kilichokuwa kinasubiriwa ni kuridhiwa na makubaliano hayo na kusainiwa kwa mkataba baina ya pande hizo mbili.

Bahati nzuri mkataba huo umesainiwa, lakini siku chache baadaye serikali kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ilitoa msimamo wao juu ya jambo hilo na kutoa mapendekezo yake ili mambo yaende sawa Jangwani.

Msimamo wa serikali sio kwa Yanga tu, bali umegusia pia mchakato wa Simba wa kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu yao kwa kutaka kumuuzia hisa za asilimia 51, mfanyabiashara maarufu na mwanachama wake Mohammed ‘MO’ Dewji. MO anataka kupewa hisa hizo kwa Sh 20 Bilioni, mchakato ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na Wana Msimbazi wanaotaka mabadiliko klabu kwao.

Hatutaki kulizungumzia sakata la Simba na MO wao, hili la Yanga ambalo tayari limeanza kuibua maneno ya chini chini kwa uongozi wa Yanga kuishutumu BMT na Kiganja kwa ujumla kwa kauli yake kwamba ni kuwaingilia. Lakini pia tayari wanachama wa Yanga wameanza kugawanyika na kuhoji juu ya mkataba huo wengi wao wakiiunga mkono serikali, kuonyesha kuwa kuna haja ya wanayanga kukaa chini na kuliangalia jambo hilo kwa umakini mkubwa bila kuruhusu mihemko.

Tunadhani kuna haja ya viongozi wa Yanga kuyaangalia yale ambayo imepewa kama muongozo na BMT kurahisisha mchakato wa mabadiliko yao katika mfumo wa klabu yao, ili kusaidia jambo hilo lifanywe kwa manufaa ya klabu na mwekezaji. Kwa mfano lipo dai kuwa, Bodi ya Wadhamini ya Yanga inayotambuliwa na Mamlaka ya Vizazi na Vifo (RITA) ni ile iliyosajiliwa mwaka 1973 ikiwa imesaliwa na majina ya watu wawili tu, Juma Mambelwa anayemiliki hati za klabu hiyo na Dk. Jabir Katundu.

Kama hilo lina ukweli hatuoni kwa nini viongozi wa Yanga wakarudi tena RITA kusajili bodi ya wadhamini mpya ili kuepusha malalamiko yasiyo ya msingi. Ni lazima Yanga itambue kuwa, BMT na Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo hakwepeki katika mabadiliko yanayotaka kufanywa ndani ya klabu hizo, ni lazima kuridhiwa na kupitishwa na wanachama wote kwa mujibu wa katiba.

 Kwa mfano wanachama wanaopinga mkataba huo wa Yanga Yetu na klabu ya Yanga wanahoji klabu hivi karibuni ilipewa kiwanja cha kujenga uwanja, lakini mkataba huo haionyeshwi na wala hawajui hati ya eneo hilo ipo wapi. Haya ni mambo yanayopaswa kutolewa ufafanuzi mapema, viongozi wasipuuze ama kuwaona wanahoji kama wakorofi.

Ndio maana tunarudia kusema mabadiliko kwa klabu zetu hayakwepeki, lakini bado viongozi wa Yanga wana muda wa kutafakari waliyoshauriwa na BMT kama yana mantiki, ili maamuzi watakayofanya yasije yakawa msalaba kwao hapo baadaye.

Pia kufanya hivyo kutasaidia kuiepusha klabu kuingia kwenye mgogoro ambao unaweza kuiweka klabu hiyo katika hali mbaya, wakati mizozo klabuni hapo ilishaanza kusahauliwa.