NYUMA YA PAZIA: Ronaldinho, nitalipia mkutano na waandishi wa habari

Muktasari:

Kisha akaendelea: “Sivutiwi na kupigana tena. Nachukia harufu ya Gym. Nachukia ngumi. Yule Tyson wa mwaka 1985, 1986 sio huyu tena. Simwoni Tyson yule tena. Sina sababu nyingine ya kuendelea kuwa katika mchezo huu. Mimi sio yule tena.

JUNI 11, 2005 katika Ukumbi wa MCI Centre jijini Washington, Marekani, bondia Mike Tyson aliwashangaza mashabiki wa ngumi duniani kote.

Kabla ya kuanza kwa raundi ya saba ya pambano lake dhidi ya bondia kibonde wa Ireland, Kevin McBride, Tyson aliamua kuondoka ukumbini.

Lilikuwa pambano lake la mwisho katika historia. Kabla ya hapo alikuwa amechapwa katika mapambano yake matatu yaliyotangulia. Historia ilikuwa inaandikwa. Mwisho wake ulikuwa umefika. Ilikuwa kama hadithi ndefu ya mapenzi ambayo mwandishi wake alikuwa anaandika sentensi ya mwisho.

Kesho yake, Tyson alikuwa akiwakabili waandishi wa habari na kuongea kwa uchungu. Alisema: “Sina tena uthubutu wa kuwa katika mchezo huu. Ningependa kuendelea lakini niliona nitapigwa. Mchezo huu haupo tena katika moyo wangu. Siwezi kuutia mchezo aibu kwa kupigwa na bondia wa aina hii (McBride). Huu ni mwisho wangu.”

Kisha akaendelea: “Sivutiwi na kupigana tena. Nachukia harufu ya Gym. Nachukia ngumi. Yule Tyson wa mwaka 1985, 1986 sio huyu tena. Simwoni Tyson yule tena. Sina sababu nyingine ya kuendelea kuwa katika mchezo huu. Mimi sio yule tena. Niliamini kuwa bado nilikuwa bondia, lakini kumbe hapana. Nimeishiwa.” Baadaye alinyanyuka akiwa na matone ya machozi na kuondoka zake.

Pamoja na ubabe wako, kuna wakati mwanadamu anafika hapa. Ndicho ninachotazamia kutoka kwa Ronaldinho wakati wowote kuanzia sasa. Kama mpaka wakati naandika makala haya hajafanya hivi, mwisho wa Ronaldinho utakuwa mbaya zaidi.

Jumanne klabu yake mpya ya Fluminense ilikubaliana na Ronaldinho kuhitimisha mkataba wake. Mkataba umekufa kwa makubaliano maalumu. Fluminense imeona kuwa Ronaldinho huyu si yule. Amecheza mechi tisa tu, ambazo ni sawa na miezi miwili.

Hajafunga bao lolote, hajapiga pasi ya bao lolote. Ni katika mechi tisa. Umewahi kufikiria Ronaldinho akicheza mechi tisa bila ya bao wala pasi ya mwisho? Tena katika ligi isiyo na mikiki mingi kama Brazil? Huyu ni Ronaldinho gani?

Ambacho kimetokea ni kwamba Fluminense wamemshukuru Ronaldinho kwa kupandisha mauzo ya jezi za timu. Mashabiki waliongezeka uwanjani na thamani ya timu iliongezeka. Tatizo Ronaldinho mwenyewe aliyesimama nyuma ya mambo haya alishindwa walau kupiga pasi ya bao katika mechi tisa.

Mashabiki wakaanza kumgeuka. Kabla ya hapo, Ronaldinho alikuwa akikipiga katika klabu ya Queretaro ya Mexico. Alisaini mkataba wa miaka miwili Septemba 2014, lakini alidumu kwa mwaka mmoja tu, tena kwa shida. Mashabiki na benchi la ufundi hawakuona umuhimu wake. Mkataba wake ukasitishwa.

Binafsi naona kuwa Ronaldinho anadhalilika. Katika umri wa miaka 35, ambayo imeambatana na starehe nyingi, Ronaldinho anadhalilika. Ni kweli kwamba ana ofa nyingi za mikataba katika klabu mbalimbali za kitajiri, lakini umefika wakati aitishe mkutano wa waandishi wa habari aongee kijasiri kama Tyson.

Wakati mwingine pesa si kila kitu maishani. Mike Tyson anakiri kwamba alipigana pambano lake la mwisho na McBride kwa sababu hakuwa na pesa ya kutumia. Lakini bado aliamua kuondoka ukumbini na kukutana na waandishi wa habari kuwaambia kuwa hawezi kudhalilika zaidi.

Kwa Ronaldinho ni tofauti. Pesa ipo. Pesa imemzunguka. Pesa haijampotea. Ana fursa nzuri ya kuvua soksi zake, akavua bukta yake na kufanya mambo mengine.

Sawa, Kwa sasa anaweza akapata dili la pesa nyingi Ligi Kuu Marekani au Qatar. Anaweza kuwafuata Frank Lampard, Steven Gerrard, Andrea Pirlo au Xavi Hernandez. Lakini bado atakuwa amekosea. Ronaldinho ni mtu tofauti na hao niliowataja. Ronaldinho ana hadhi yake ya juu zaidi.

Ukienda kumtazama Ronaldinho bado utafikiria kupata makubwa kutoka kwake. Ni tofauti na Lampard ambaye aina yake ya soka inaeleweka kuwa ni ya matokeo zaidi. Kwa Ronaldinho utataka vitu ambavyo kama hawezi kuvitoa tena basi ina maana anakuwa tapeli wa mchana na anajidhalilisha.

Mike Tyson angeweza kuja hata Afrika kupigana na akapata kiasi fulani cha pesa, lakini angekuwa anajidhalilisha kama angeanza kupigwa na mabondia wa aina ya McBride. Mwenyewe alilijua hilo na ndiyo maana akatupa taulo na kuondoka zake pale ukumbini MCI Centre.

Dunia iliuona mwisho wa Pele, mwisho wa Diego Maradona, mwisho wa Zinedine Zidane, mwisho wa Ronaldo de Lima. Haitashangaa sana kuuona mwisho wa Ronaldinho. Haitashangaza. Mambo hufika mwisho. Ni wakati wa kuitisha mkutano wa waandishi wa habari. Hata mimi mwenyewe naweza kulipia mkutano wake na waandishi wa habari. Ronaldinho aliyewafunga Chelsea huku akikata viuno sio wa kucheza mechi tisa za Ligi Kuu Brazil bila ya bao wala pasi ya mwisho.

Ronaldinho aliyewafanya mashabiki wa Santiago Bernabeu wasimame na kumpigia makofi baada ya kuwafunga mabao mawili ya ajabu, hawezi kudhalilika hivi.