Ishu inayomponza Mzamiru

Muktasari:

Mzamiru aliyejiunga na Simba Juni 2016 akitokea Mtibwa Sugar, anaelekea ukingoni mwa mkataba wake klabuni hapo na tayari amehusishwa na timu za Yanga na Zamalek ya Misri jambo ambalo limewakera mabosi wake.

IMEFICHUKA kuwa zile harakati za kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin kutaka kuihama timu hiyo mwishoni mwa msimu, zimemponza na kumfanya aanze kusugua benchi Msimbazi.

Mzamiru aliyejiunga na Simba Juni 2016 akitokea Mtibwa Sugar, anaelekea ukingoni mwa mkataba wake klabuni hapo na tayari amehusishwa na timu za Yanga na Zamalek ya Misri jambo ambalo limewakera mabosi wake.

Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu na staa huyo zimesema mmoja wa mabosi wa Wekundu wa Msimbazi hao alimwambia Mzamiru kwamba kwa kuwa ameonyesha nia ya kuondoka, ni vyema akasugua benchi na kuwapisha nyota wengine wenye nia ya kusalia klabuni hapo wacheze.

Mzamiru amekuwa akisugua benchi kwenye mechi za karibuni hasa baada ya ujio wa kocha Mfaransa, Pierre Lechantre. Enzi za kocha Joseph Omog, kiungo huyo alikuwa hakosekani kikosi cha kwanza.

Kitendo cha staa huyo kukaa benchi ni kama kinapunguza makali ya mkataba atakaosaini mwishoni mwa msimu kwenda timu yoyote tofauti na staa mwenzake, Shiza Kichuya ambaye anacheza mara kwa mara.

Kichuya na Mzamiru wamekuwa wachezaji muhimu ndani ya Simba tangu walipojiunga na timu hiyo mwaka juzi, na kuisaidia kubeba taji la FA mwaka jana pamoja na kumaliza nafasi ya pili Ligi Kuu.

WADAU WANENA

Meneja wa Mbwana Samatta, Jamal Kasongo, amesema thamani ya kiungo huyo haiwezi kupotea kirahisi kutokana na upambanaji wake, ila amemtaka aendelee kuwa mbunifu zaidi uwanjani.

“Kitu kimoja nilichokiona kwa Mzamiru ni mchezaji mpambanaji, lakini aongeze ubunifu, amtazame Said Ndemla alikuwa anasugua benchi, lakini kwa sasa amekuwa mzuri mara dufu kwa kuwa ni mbunifu,” alisema.

Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema Mzamiru na Kichuya wakitaka kufika mbali, lazima wawe na nidhamu ya hali ya juu na wasijione wamefika.

“Nidhamu itawafanya wafikie malengo yao, licha ya kwamba Mzamiru kwa sasa hachezi bado anapaswa kujiuliza nini afanye yaani amlazimishe kocha kumpanga kwa uwezo na si maneno,” alisema.