Dili jipya Yanga kumbe hivi

YANGA imesaini mkataba na kampuni ya vifaa vya michezo ya Macron itakayowapatia zaidi ya Sh2 bilioni kwa muda wa miaka mitatu, lakini sasa kama hujui dili hilo jipya lina vipengele fulani ndani yake vinavyoifanya Yanga itishe ikiwaacha mbali watani zao Simba.

Halafu sasa ni kwamba Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, kwa kusaini mkataba huo imewafanya wawe na mikataba miwili minono baada ya mwaka jana kusaini na SportPesa inayowapa Sh950 milioni kwa msimu huu huku fedha hizo zikipanda kila msimu. Simba wao na ujanja wao wote wana mkataba wa SportPesa tu na wanavuna kiasi kama hicho inachochukua Yanga, hivyo dili hilo jipya la Jangwani linawafanya Yanga waiache mbali Simba kama utani.

Kwa mujibu wa mkataba wa Yanga na Macron, mbali ya timu hiyo kupewa zaidi ya Sh660 milioni kila mwaka, bado kuna mambo makubwa zaidi ambayo wanatakiwa kufanyiwa na kampuni hiyo.

Inaelezwa kuwa mbali na fedha hizo ambazo lazima Yanga wapewe kila mwaka, watakuwa pia wakipata mgawo wa asilimia 30 ya faida kutoka kwenye mauzo ya vifaa vyenye nembo yab klabu hivyo ambapo hesabu itakuwa ikifanywa kila baada ya miezi mitatu.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba Macron imepanga kuagiza jezi 500,000 tofauti ili kuziuza na endapo zitakwisha Yanga itakuwa imepiga pesa za maana unaambiwa.

Kigogo mmoja wa Yanga aliyeombwa kuhifadhiwa jina lake, alisema klabu hiyo pia itakuwa ikipewa vifaa vya kutumia kwa kila msimu, ambapo kila mchezaji atapewa jezi sita za nyumbani, sita za ugenini na nyingine sita za mechi za kimataifa hivyo kila mmoja kuwa nazo 18.

Timu hiyo pia itapewa mipira 150 kwa ajili ya mazoezi ya mechi. Jezi moja ya Yanga itakuwa ikiuzwa kwa Sh16,000 na 20,000 huku zile zinazovaliwa na wachezaji zikiuzwa kwa Sh50,000.

“Kama biashara itakwenda vizuri, Yanga itakuwa ikipata fedha nyingi zaidi hata ya za SportPesa, kikubwa ni usimamizi na mikakati,” alisema kigogo huyo.

Aliongeza kuwa mipango ya kusaka wadhamini zaidi inaendelea ili Yanga iondokane na maisha ya kuungaunga.