De Bruyne ujanja uwanjani tu

Muktasari:

Kiungo huyo kwa sasa ndiye anayesifika kwa kupiga pasi nyingi za mabao ya Man City

MANCHESTER, ENGLAND. HAKABIKI. Ndivyo unavyoweza kumzungumzia staa wa Manchester City, Kevin de Bruyne, kutokana na kandanda analopiga msimu huu.

Staa huyo wa zamani wa Genk aliondoka kwenye Ligi Kuu England kwa miaka mitatu alipokwenda Ujerumani kabla ya kurudi England akiwa moto kweli kweli.

Mara yake ya kwanza alipokuwa England, alionekana kama ni nyongeza tu huko Chelsea chini ya Jose Mourinho, lakini kwa sasa amewasha moto kwenye kikosi cha Man City na kama wanatajwa wachezaji mahiri wa msimu huu, basi litatajwa jina lake na la Mohamed Salah wa Liverpool.

Wakati ukiendelea kushangaa vitu vya KDB anavyofanya ndani ya uwanja, cheki na haya mambo usiyoyafahamu kuhusu fundi huyo wa mpira.

Aporwa demu na kipa wa Chelsea

KDB na kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois, wote ni Wabelgiji, lakini wawili hao waliingia kwenye bifu kubwa kisa mwanamke, mrembo Caroline Lijnen.

KDB alibainisha hilo kwenye kitabu chake cha mwaka 2014 kilichoitwa kwa jina la Keep It Simple, akielezea alivyoingia kwenye bifu kubwa na Courtois baada ya kuporwa demu wake.

“Demu wangu alikwenda Madrid na marafiki zake na huko akawa na uhusiano na Thibaut,” aliandika KDB kwenye kitabu hicho. Lakini, mrembo huyo alidai De Bruyne ndiye aliyeanza kumsaliti, hivyo yeye alilipa tu kisasi.

Aanzisha mavazi kuchangisha pesa

Wanasoka wa kizazi cha sasa wana kampuni zao za mitindo ya mavazi ikiwa ni sehemu tu ya kujiongezea kipato, lakini kwa KDB alifanya hivyo ili kuchangisha pesa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii, kuwasaidia wasiojiweza.

Akiwa Balozi wa Olimpiki Maalumu, kampuni ya mavazi ya staa huyo ilianza mwaka 2014 na lengo lilikuwa kuchangisha pesa kusaidia wenye mahitaji maalumu. Kitu muhimu ni kwamba mwitikio umekuwa mkubwa ambapo mavazi yenye lebo ya KDB yamepata wanunuzi wa kutosha na kuingiza pesa zinazofaa kwenye kusaidia wenye uhitaji.

Wenzake wamwita kauzu

Mastaa wenzake na Kevin De Bruyne wamekuwa wakimuita staa huyo kuwa kauzu kutokana na namna asivyopenda kufichaficha mambo na kumweleza mtu bayana akiona amekosea au anapohitaji jambo lake kuwa.

KDB ni mtu mtaratibu sana, lakini huwa anasema anachokifanya. De Bruyne amekuwa mtu wa kusisitiza kutaka yake yafanyike na ndiyo maana hata anapokuwa ndani ya uwanja, kitu cha kwanza anachohitaji ni timu yake kushinda.

Anapenda sana wanyama

Kitu pekee ambacho KDB amekuwa akipenda kukifanya basi ni kwenda kwenye mbuga kutazama wanyama na hasa ndege. Kutembelea mbuga au hifadhi ya wanyama ni kitu anachokipenda zaidi kiungo huyo mchezeshaji na mara nyingi amekuwa akihusishwa katika uhifadhi wa mazingira ili kufanya kile anachokipenda kuendelea kuwa hai.

Mwaka 2014 alichaguliwa kuwa Balozi wa Ndege huko Walsrode, Ujerumani ambako kuna aina 675 za ndege.

Anaruhusiwa kuichezea Burundi kimataifa

Ilibaki kidogo tu kulichezea taifa hilo la Afrika katika soka la kimataifa, kwani ana ruhusa hiyo. Mama yake (Anna De Bruyne) alizaliwa Burundi kabla ya kwenda Ivory Coast na kisha England, ambako alitumikia sehemu kubwa ya maisha yake ya utotoni.

Mwanzoni, wakati De Bruyne yupo Genk ilielezwa kwamba anaweza kufuzu kuichezea England, lakini hiyo ingelazimishwa tu, mahali alikozaliwa mama yake staa huyo ni Burundi, hivyo KDB angeruhusiwa kulitumikia taifa hilo kwenye soka la kimataifa.

Hata hivyo, Burundi ingemfanyia nini staa mwenye kipaji kama KDB kwa sababu haijawahi kufuzu Kombe la Dunia na hata Kombe la Mataifa ya Afrika ni mtihani mzito kwao.