Azam yaiteremsha Simba kileleni

Muktasari:

Azam yafikisha pointi 30 na kuishusha Simba yenye pointi 29 hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Mbeya. Maafande Tanzania Prisons wameshindwa kuutumia uwanja wao wa nyumbani na kujikuta wakichezea kichapo cha bao 2-0 dhidi ya Azam FC.
Mechi hiyo ambayo imechezewa Uwanja wa Sokoine Mbeya ilikuwa na upinzani mkali kwa timu zote kuanzia kipindi cha kwanza kwa timu zote kufanya mashambulizi ya mara kwa mara.
Lakini ya mabeki wa Prisons yamewapa mwanya wa wachezaji wa Azam kuzitumia vizuri nafasi mbili ambazo zimewapatia ushindi huo wa pointi 3 muhimu.
Bao la kwanza la Azam lilipatikana dakika ya 7O kupitia kwa Yakub Mohammad aliyefunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa na  Salmin Hoz wakati bao la pili lililozima kabisa ndoto za maafande hao, lilifungwa na Paul Peter baada ya kupata pasi kutoka kwa  Yahaha Dayd dakika ya 83.
Hata hivyo mabeki wa Prisons walionekana kujutia makosa yao yaliyoruhusu mabao hayo.
Kipindi cha kwanza kilianza huku manyunyu ya mvua ambayo ilinyesha kwa takriban dakika 30 jambo lililowafanya wachezaji kushindwa kumudu mpira ipasavyo.