Arsenal yapewa AC Milan

Nyon, Uswisi. Arsenal imepangwa kucheza na AC Milan katika hatua ya 16 ya Europa Ligi.

Mashabiki wa Arsenal watakuwa na safari ya San Siro usiku wa Alhamisi wa Machi 8, kabla ya kurudiana kwenye Uwanja wa Emirates, Alhamis ya Machi 15.

AC Milan inayofundishwa na kiungo wa zamani wa Rangers na Italia, Gennaro Gattuso aliyechukua jukumu hilo Novemba mwaka jana baada ya kutimuliwa kwa  Vincenzo Montella.

Milan kwa sasa ipo nafasi ya saba katika Serie A, ikiwa nyuma kwa pointi 25, kwa  vinara wa Napoli, lakini si timu ya kubeza.

Milan imekuwa na rekodi nzuri katika siku za karibuni ikiwa haijafungwa katika mechi 10, pamoja na ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Ludogorets ya Bulgaria usiku wa jana na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-0.

Vijana wa Arsene Wenger walifungwa na timu ndogo ya Sweden, Ostersunds FK, lakini wamefanikiwa kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2

Wenger alisema "hatukujua tunacheza nini uwanjani" baada ya kufungwa 2-1 nyumbani na timu iliyoanzishwa 1996 na kucheza daraja la nne kwa miaka saba chini ya kocha Muingereza Graham Potter.

Miamba ya Russia, Zenit St Petersburg iliyowatoa mabingwa wa Scotland, Celtic wamepangwa kucheza na RB Leipzig ya Ujerumani.

Ratiba kamili ya Europa Ligi 16 bora:

Lazio v Dynamo Kiev; RB Leipzig v Zenit St Petersburg; Atletico Madrid v Lokomotiv Moscow; CSKA Moscow v Lyon; Marseille v Athletic Bilbao; Sporting Lisbon v Viktoria Plzen; Borussia Dortmund v Red Bull Salzburg na AC Milan v Arsenal