Ajibu, Chirwa utawapenda

Muktasari:

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 46 na kulingana na Simba, ikizidiwa mabao 11 na watani wao, Simba waliopo kileleni wakiwa pia na mchezo mmoja mkononi, Chirwa akifikisha bao lake la 12 na Ajibu la saba msimu huu.

KAMA utani vile, Yanga imeinasa Simba kiulaini katika mbio zao za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, baada ya jana Jumatatu kupata ushindi wake wa tisa mfululizo kwa kuinyuka Stand United mabao 3-1, huku Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa wakiendelea kutakata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 46 na kulingana na Simba, ikizidiwa mabao 11 na watani wao, Simba waliopo kileleni wakiwa pia na mchezo mmoja mkononi, Chirwa akifikisha bao lake la 12 na Ajibu la saba msimu huu.

Katika mchezo huo, Yanga iliingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Stand katika mechi yao ya kwanza na kuandika bao la kuongoza dakika ya saba kupitia Yusuf Mhilu aliyemfinya beki Miraj Maka na kupiga mpira uliosindikizwa wavuni na Ally Ally.

Ajibu aliendeleza makali yake kwa kuandika bao la pili dakika ya 12 kwa bao tamu baada ya kumegewa pande safi na Maka Edward na yeye kuupiga kiufundi mpira huo uliotinga nyavu ya pembeni na kumuacha kipa Mohammed Makaka akiduwaa.

Kipindi cha pili ndicho kilichokuwa kitamu na hasa baada ya Stand kurudi kivingine na kuikimbiza Yanga kabla ya kupata bao la kufutia machozi dakika ya 84 kupitia Vitalis Mayanga, akimalizia krosi pasi ya Aaron Lulambo. Hata hivyo, bao hilo lilidumu kwa dakika mbili tu kabla ya Chirwa kukwamisha la tatu akimchambua kipa Makaka.

Licha ya ushindi, lakini Yanga jasho liliwatoka kwa Stand iliyosaliwa nafasi ya 11 ikiwa na alama zao 22 kwa kucheza mechi 22.

LWANDAMINA ASHITUKIA CAF

Kocha wa Yanga, George Lwandamina ameziangalia rekodi za Yanga kabla na baada ya kujiunga nayo akitokea Zesco United ya kwao, kisha akawauma sikio mabosi wake.

Kwa muda mrefu sasa Yanga imekuwa ikisaka mafanikio kwenye michuano ya kimataifa, lakini mara nyingi inakwama njiani na Lwandamina ameibua sababu ya mabingwa hao kuchemsha.

Mzambia huyo aliamua kuitisha kikao kizito na mabosi wake na kuwaeleza wazi ni lazima mambo matatu yafanyike haraka kabla ya msimu mpya kuanza, kama kweli wanataka itambe kimataifa na kuvuna mabilioni ya fedha kutoka CAF.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika, alilieleza Mwanaspoti kuwa, Lwandamina na wasaidizi wake wamewapa mchongo baada ya kushtukia sababu za kuchemsha kimataifa.

Alisema Mzambia huyo ameitaka Yanga kubadilika na kuendana na maisha ya klabu kubwa Afrika, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha za maana kama posho za wachezaji wanaposhinda mechi za kimataifa ili kuwapa mzuka na kujituma.

Yanga imetakiwa kutenga posho kubwa za wachezaji katika mechi za kimataifa kuliko za ndani, akisema ndio inazifanya timu kubwa kutamba kwa kutumia mbinu hizo za kijanja.

Mbinu hiyo inatajwa kuwa kutumiwa na Township Rollers ya Botswana, ambayo mwishoni mwa wiki hii watakutana nao katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa, ambao Yanga inahitaji ushindi ili kusonga mbele. Kwenye mchezo wa kwanza wageni hao kupitia rais wa klabu yao Jagdish Shah, waliwatengea wachezaji wao mamilioni, ambapo kila mmoja aliahidiwa dola 5,000 (sh 11.2 milioni) kama wataibuka na ushindi wakati Yanga walikuwa kimya.

“Ametaka tuboresha posho za wachezaji ziwe na uzito kwa kuwa, huku ndiko kuna fedha za maana kuisaidia timu,” alisema Nyika na kuongeza: “Hilo tumelikubali kwa kuwa ametupa mpaka mifano, tuangalie katika mechi za ligi kuna posho kwa wachezaji wakishinda, lakini huku CAF hatuna kitu ambacho ni tofauti na klabu kubwa za Afrika.”

Bosi huyo, ambaye pia anaongoza kamati ya usajili alisema mbali na hilo, Lwandamina ametaka msimu ujao kuweka vipengele kwenye mikataba ya wachezaji ili kurudisha nidhamu na uwajibikaji.

“Mchezaji atatakiwa kufanya kazi kulingana na mkataba wake na akikiuka adhabu yake iwepo wazi, hili limetupa picha halisi ya tofauti ya wachezaji wa nje wanapokuja hapa tunaona tofauti,” alisema.

Pia, Mzambia huyo ametaka kufanyika maboresho makubwa kwa nyota wa kikosi hicho kwa kuletwa wachezaji wenye ushindani ili kuifanya timu kuwa imara.