Vichwa 12 Yanga vyakabidhiwa Simba

Muktasari:

Mabosi hao wa Yanga wameunda Kamati ya Mashindano yenye wajumbe 12 na kuwapa jukumu la kuhakikisha wanaimaliza Simba katika mechi zao, sambamba na kuhakikisha wanatetea ubingwa wa Bara na kutamba anga za kimataifa.

YANGA bado haijajua itaweka wapi kambi yake ya mazoezi kujiandaa na msimu mpya wa mashindano, lakini katika kuhakikisha inaimaliza Simba mapema, uongozi wa juu ya klabu hiyo umeteua vichwa 12 na kuwakabidhi kazi maalumu.

Mabosi hao wa Yanga wameunda Kamati ya Mashindano yenye wajumbe 12 na kuwapa jukumu la kuhakikisha wanaimaliza Simba katika mechi zao, sambamba na kuhakikisha wanatetea ubingwa wa Bara na kutamba anga za kimataifa.

Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alifanya uteuzi wa kamati hiyo jana Jumatano na badiliko kuu likimhusu Mwenyekiti, Mhandisi Paul Malume ambaye amepewa mapumziko na nafasi yake kuchukuliwa na Majid Suleiman.

Licha ya Sanga kutoweka wazi sababu za mabadiliko hayo, japo Mwanaspoti linafahamu, Malume ameondolewa baada ya kwenda kusoma hivyo kushindwa kuwa karibu na kamati hiyo ambayo wajumbe wake wengi ni matajiri wakubwa.

Katika uteuzi huo, Makamu Mwenyekiti anaendelea kuwa Mustapha Urungo lakini Katibu Mkuu atakuwa Urio Edward badala ya Samuel Lukumay aliyekuwepo hapo awali. Lukumay ataendelea kuwa mjumbe wa kawaida.

Wajumbe wengine ni Rodgers Gumbo, Omary Chuma, Yanga Makoga, Lameck Nyambaya, Hussein Nyika, Edgar Mutani, Leonard Chinganga na Yusuf Mohammed.

Mtihani wa kwanza mkubwa wa kamati hiyo utakuwa kuhakikisha Yanga inaifunga Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 23 kabla ya kufanya mambo kwenye mechi za Ligi Kuu Bara itakayoanza Agosti 26.

Majukumu mengine ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ambapo mwakani Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, licha ya kuwa na kibarua cha kufanya vema katika Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi.

DANTE NA UBINGWA

Katika hatua nyingine, beki Andrew Vincent ‘Chikupe’ amekiangalia kikosi chao kilivyo na kutamka kuwa ni lazima wachukue ubingwa tena kutokana na kuanza maandalizi ya mapema na kocha Lwandamina aliyewapa taji la tatu mfululizo.

Dante alisema kuwa kocha huyo katika msimu uliopita aliingia katikati, lakini aliweza kuifanya Yanga ikawa mabingwa licha ya kuwa alikuwa hawafahamu wachezaji vizuri, lakini kwa msimu mpya itakua ubingwa mapema zaidi.

“Msimu uliopita nakumbuka alikuja katikati na wala alikuwa hatujui sana wachezaji mmoja mmoja, lakini aliweza kuifanya timu ikachukua ubingwa, sasa hivi tumeanza naye mapema kwa hiyo nina imani tutafanya vizuri katika ligi hata mashindano ya kimataifa,” alisema.

Akizungumzia maandalizi yake binafsi kipindi cha mapumziko, alisema kuwa aliamua kuanza kujitengeneza na maandalizi ya ufukweni, kutokana na kukaa nje muda mrefu kipindi yupo majeruhi hivyo aliamua kujitengeneza ili kuwa sawa na wenzake.

“Nilikaa nje kwa muda mrefu na hata ligi sikumalizia, lakini niliamua kuanza na mazoezi ya mchangani ili kujiweka sawa, yalinisaidia nikacheza SportPesa na hata hivi sasa katika gym naona nipo vizuri, mapumziko yangu sikukaa bure niliyatumia vizuri,” alisema.

Aliongeza kuwa anatambua ugumu wa namba ambao atakutana nao, lakini hilo anamuachia kocha aamue kutokana na msimu uliopita anaamini kilichokuwa kinamweka nje ni majeruhi na hivi sasa yupo fiti kwa ajili ya msimu ujao.

KAMUSOKO, KABWILI

Yanga pia jana Jumatano iliwasainisha mikataba kiungo, Thaban Kamusoko na kipa wa Serengeti Boys, Ramadhan Kabwili.

Kamusoko ambaye alijiunga na Yanga mwaka 2015 ameongeza mkataba wa miaka miwili wakati Kabwili aliyeng’ara na Serengeti akisaini mkataba wa miaka mitano.

Usajili huo ulifanyika mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika na Katibu Mkuu wa klabu, Charles Mkwasa.