Kessy, Gadiel kuamua ushindi wa Yanga

Muktasari:

Katika mazoezi ya jana kocha wa Lwandamini alikuwa akifanyia kazi mfumo wa 3-5-2 ambao ni wazi Kessy na Gadiel wana majukumu ya kulinda na kushambulia hasa kwa kupiga mipira ya krosi dhidi ya St Louis.

Victoria, Shelisheli. Kocha wa Yanga, Geogre Lwandamina amewapa majukumu ya ziada mabeki wake Hassani Kessy na Gadiel Michael katika kuhakikisha wanashinda mechi ya kesho dhidi ya St Louis ya Shelisheli.

Katika mazoezi ya jana kocha wa Lwandamini alikuwa akifanyia kazi mfumo wa 3-5-2 ambao ni wazi Kessy na Gadiel wana majukumu ya kulinda na kushambulia hasa kwa kupiga mipira ya krosi dhidi ya St Louis.

Katika mfumo huo, mabeki hao watapaswa kuingia ndani kwenye eneo la katikati St Louis itakapokuwa na mpira, pia itapaswa kutanua uwanja na kucheza kama viungo wa pembeni Yanga itakapokuwa inashambulia.

Akizungumzia mfumo huo, Kessy alisema ni mzuri na utawasaidia kuwaweka katika mazingira magumu wapinzani wao.

"Mchezaji mpira ni kama askari muda wote anatakiwa kuwa tayari kutimiza majukumu atakayopangiwa. Kama kocha ameamua tucheze hivi nadhani tunalazimika kutimiza majukumu yetu ipasavyo ilimradi timu ifanikiwe kupata inachokitaka.

“Binafsi nipo tayari kucheza katika nafasi yoyote ile ambayo kocha atanipanga. Kinachotakiwa ni timu kupata matokeo na sio mchezaji anacheza wapi au nani kapangwa au hajapangwa," alisema Kessy.

Kessy amechukua nafasi ya Juma Abdul katika nafasi ya beki wa kulia katika mechi za hivi karibuni baada ya mchezaji huyo kupata majeraha.