Yanga yaichapa Stand United

Muktasari:

Yanga ndiyo timu iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nyingi zaidi 27

Dar es Salaam.Yanga imefuata Simba kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kuichapa Stand United kwa mabao 3-1 mbele ya mashabiki wachache waliojitokeza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo mabao ya Yanga yalifungwa na  Ibrahim Ajib, bao la kujifunga kwa beki wa Stand United, Ali Ali na Obrey Chirwa huku Vitalis Mayanga akifunga bao la kufutia machozi kwa Stand.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 46, sawa na Simba inayoongoza kwa tofauti ya mabao wakati timu hizo mbili zikigeukia katika mashindano ya kimataifa mwishoni wiki.

Yanga ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza katika dakika ya sita alilojifunga beki wa Stand United, Ali Ali wakati akizuia krosi ya Yusuf Mhilu.

Wakati Stand United ikijuliza mshambuliaji Ajib alifunga bao la pili dakika 14 akitumia vizuri pasi ya Chirwa mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Stand United walirudi kwa nguvu na kulishambulia lango la Yanga, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini.

Kasi hiyo ya mashambulizi ya Stand United yalizaa matunda na kufanikiwa kupata bao lililofungwa na Vitalis Mayanga katika dakika 84.

Yanga ilipata bao la tatu lililofungwa na Chirwa baada ya kutumia vizuri makosa ya mabeki wa Stand United na kupiga shuti lililojaa wavuni katika dakika 85.

Pamoja na Yanga kurudi kwa kasi katika mbio za ubingwa bado mechi zake zimeshindwa kuwavutia mashabiki wake.

Yanga imeshinda michezo yake saba ya Ligi Kuu bara, lakini aina ya kikosi chake kilichojaa chipukizi kwa sasa imeshindwa kuwavutia mashabiki wa mabingwa hao kujitokeza kwa wingi uwanjani.

Yanga inayosifika kwa kuwa na mashabiki wengi nchini msimu huu imeshindwa kuvutia mashabiki wake na hata wale waliopo uwanjani wanaonekana kutokuwa na shamla shamla kama ilivyozoeleka.

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa kati ya Yanga na Township Rollers ya Botswana ni mashabiki 9,961 tu walioshudia mechi hiyo na kuingiza Sh 56.2 milioni.

Wakati watani zao Simba mechi yake ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Masry uliofanyika usiku ulishudiwa na mashabiki 14,798 na kuingiza Sh 85 milioni.