Mourinho ageuka mbogo kwa madaktari kisa Herrera

Muktasari:

Man United watalazimisha kushinda mechi ya marudiano nyumbani ili kujihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa

SEVILLE, HISPANIA. Katika hali ya kuanza kuchanganyikiwa kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amekuwa mkali kwa madaktari wake kwa kumfanya afanye makosa katika uchaguzi wa kikosi chake kilicholazimisha suluhu dhidi ya Sevilla katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mechi hiyo, Mourinho alimwaanzishia benchi kiungo Paul Pogba na kumpanga Ander Herrera baada ya kuhakikishiwa na madaktari kwamba mchezaji huyo yupo fiti, lakini baada ya dakika 17 tu Mhispaniola huyo hakuweza kuendelea na mechi.

Jambo hilo lilimfanya Mourinho kufanya mabadiliko ya mapema kwa kumwingiza Pogba, lakini huko haikuwa mpango wake wa kufanya mabadiliko ya mapema hivyo na kuamua kuwasema madaktari wake kwamba wamefanya makosa.

Herrera hakuwa amecheza kwa mechi tatu mfululizo baada ya kuripotiwa kuwa majeruhi.

Mourinho alisema: "Nadhani atakuwa amepata majeraha mabaya. Alikuwa na tatizo kidogo lililomfanya akose mechi kadhaa zilizopita, lakini kitendo cha madaktari walisema kwamba yupo fiti kwa asilimia 100.

"Tusingemchezesha hapa na tungempa mapumziko zaidi kupona. Ukweli hakuwa fiti, lakini nashangaa madaktari kusema yupo fiti."

Wababe hao watarudiana wiki mbili zijazo huko Old Trafford kupata timu moja itakayotinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.