Yanga yaipa presha Kagera Sugar

Muktasari:

Mara ya mwisho kwa Yanga  na Kagera Sugar kukutana ilikuwa ni Januari 15 kwenye uwanja wa Uhuru jijini ambapo Yanga ilichapwa mabao 3-0.

Matokeo ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga, yameipa Kagera Sugar wasiwasi kuwa yatachochea ugumu wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini mnamo Januari 15 mwaka huu, Yanga ilichapwa mabao 3-0.

Akizungumza na Mwanaspoti Online,Kyaruzi alisema anajua mchezo huo utakuwa mgumu kwao kutokana na Yanga kutaka kulipiza kisasi lakini wamejipanga kuwakabili.

“Huu mchezo tunajua utakuwa mgumu sana Yanga watakuja na hasira ya kulipiza kisasi kwani kwenye mchezo wa Ligi tuliwafunga 3-0 kitu ambacho kitafanya waingie kwa kasi katika huo mpambano.

Tutakachokifanya tutawakabili kwani tuko fiti kabisa katika hili pambano na tunahitaji sana ushindi hivyo wala hatuna hofu na huu mchezo kikubwa tutakuwa makini nao,” alisema Kyaruzi.

Beki huyo aliyecheza mechi 27 mpaka sasa za Ligi Kuu alisema msimu huu nao wamejipanga kuweza kufanya vizuri kwenye kombe hilo kwani mipango yao kwanza ni kutinga fainali kisha kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

“Mashabiki wetu tunaomba sapoti yao katika huu mchezo hatutoweza kuwaangusha tutapambana kuweza kupata ushindi kwani malengo yetu ni kuona tunatinga fainali kisha tutapiga sasa hesabu za ubingwa,” alisema Beki huyo wa zamani wa Toto Africans na Mbeya City.

Hisia hizo za kisasi ambazo zimewapa hofu Kagera Sugar zinaonekana kuwepo hata upande wa Yanga ambao kupitia kocha wao, Luc Eymael wameonyesha nia ya kutaka kulipa kisasi.

"Nakumbuka tulipoteza dhidi ya Kagera Sugar na kipindi kile mimi nilikuwa ndio naanza kuifundisha timu.

Ni mechi ambayo itakuwa ngumu lakini kwa upande wetu tumejiandaa vizuri na shabaha yetu ni kuibuka na ushindi katika mchezo huo," alisema Eymael.