Wachezaji Yanga wataka fedha za changia walipwe mishahara

Thursday April 25 2019

 

By Charity James

Dar es Salaam. Wachezaji wa Yanga wameweka wazi sababu zilizowafanya wasusie mazoezi leo asubuhi kuwa uamuzi wa uongozi kukusanya fedha kwa ajili ya usajili ujao wakati wao wanadai mishahara.

Wachezaji hao wakizungumza na mtandao wa Mwanaspoti kwa sharti la kutotaka majina yao kuandikwa walisema wakati changia Yanga likiendelea chini ya Mwenyekiti Anthony Mavunde lililozinduliwa Dodoma likiwa na lengo la kuhakikisha wanakusanya Sh 1.5bilioni ili kuboresha kikosi chao msimu ujao nyota wa timu hiyo wameibuka na kuumizwa na kampeni hiyo.

Walisema wanaumizwa na uamuzi unaofanywa na kampeni hiyo kulenga zaidi usajili wa msimu ujao wakati wao wanateseka hawana malipo ya mishahara.

Walisema wanadai pesa zao za mishahara ya miezi mitatu wanapambana kuhakikisha wanapata matokeo katika kila mchezo, lakini bado hawapewi kipaumbele zaidi wanasikia kuna michango inatolewa lakini haiwahusu inalengo la kufanya usajili.

Pia, walidai kuwa Kocha wao Mwinyi Zahera walimuomba leo awaletea viongozi katika mazoezi ya asubuhi ili wajadiliane juu ya stahiki zao, lakini hawakufika ndipo walipoamua kuchukua uamuzi huo.

"Tulifika mazoezini, lakini hatujafanya mazoezi kitu kikubwa kilichokwamisha mazoezi hayo ni kushindwa kutokea kwa kiongozi hata mmoja mazoezini kama tulivyokuwa wakitegemea ndipo tulipokwazika na kukubaliana kuondoka bila kufanya mazoezi."

Advertisement

"Kocha Zahera alionyesha msimamo wa kutotaka kujadiliana chochote na sisi zaidi ya kutuamrisha tuingie uwanjani kufanya mazoezi hatukufanya hivyo hadi tulipochukua uamuzi wa kuondoka," walisema.

Mwanaspoti lilimtafuta Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omar Kaaya kuzungumza hali hiyo simu yake iliita bila kupokelewa hadi gazeti hili linapelekwa mtamboni.

 

Advertisement